
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kujenga Barabara ya Bigwa- Mvua- Kisaki pamoja na kukamilisha ujenzi wa barabara ya Ubena- Zomozi- Ngerengere ndani ya miaka mitano ijayo ikiwa atapata ridhaa ya kuwaongoza Watanzania kupitia uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Wakati wa Siku yake ya kwanza ya Kampeni Mkoani Morogoro leo Ijumaa Agosti 29, 2025, Rais Samia pia ameahidi kuimarisha huduma za afya Wilayani humo, kwa kujenga vituo viwili vipya vya afya, zahanati saba, kukamilisha ujenzi wa zahanati nne unaoendelea sasa hivi, akihamasisha pia wananchi kujiunga na Bima ya afya.
"Tunataka watu wote na watu wetu wa Ngerengere hatuna sababu ya kutojiunga na bima ya afya, nimesema hapa kuwa mazao tuliyouza msimu uliopita yameleta Bilioni 11 mikononi kwa wakulima, Wafugaji nao Alhamdulillah senti zinaingia mkononi, ni kutumia fedha kidogo kununua bima yako ya afya wewe na familia na mkaendelea kupata matibabu kwa mwaka mzima." Amesema Rais Samia.
Katika hatua nyingine Dkt. Samia pia ameahidi kuwa ikiwa atachaguliwa, Serikali yake itajenga maghala mapya matatu na kuendelea kuzalisha na kutoa miche ya karafuu, Kokoa na Michikichi pamoja na kuanzisha vituo viwili vya kukodisha zana za kilimo ili kumpunguzia Mkulima gharama kubwa za uzalishaji wa mazao ya kilimo.
No comments:
Post a Comment