Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Shirika la mtandao wa jinsia Tanzania ( TGNP) limeendelea kutekeleza mradi wa wanawake wa vijiji kuleta mabadiliko ( rural women cultivating change- RWCC) wenye lengo la kumkomboa mwanamke katika nyanja mbalimbali ikiwemo kilimo ikolojia.
Hayo yamebainishwa Agosti 6,2025 na Mratibu wa mradi huo Bi.Catherine Kasimbazi wakati akizungumza na Sema swahili Blog katika maonesho ya nanenane Nzuguni,Jijini Dodoma ambapo amesema mradi huo kwa sasa unatekelezwa katika mikoa mitatu ambayo ni Manyara,Kilimanjaro na morogoro.
"Mradi wa Rural Women Cultivating change unaangalia wanawake na uongozi katika suala la kilimo maana wanawake wanaonekana kuwa nyuma katika kufanya maamuzi,pia mradi huu unalenga kuwakomboa wanawake katika suala la unyanyasaji wa kingono.
" Kama tunavyojua kuwa kilimo ikolojia ni kilimo stamilivu katika maeneo ya jamii zetu na sisi tumekuwa tukiwahamasisha wanawake hawa kutumia mbegu asili,hapa tunawaelekeza namna nzuri ya kutumia mbegu hizo katika kukuza hiki kilimo ikolojia,"amesema.
Amesema kupitia mradi huo, 'TGNP' imeweza kuwafikia wanawake zaidi ya 2,000 na kuhakikisha wananufaika na kilimo cha kutumia mbegu asili.

Naye mmoja wa wanufaika wa mradi huo wa 'RWCC' Bi.Clara Male kutoka mkoa wa Manyara amesema mradi huo umekuwa mkombozi kwa wanawake wengi kwani hujitengenezea mbegu za mazao wenyewe jambo linalopunguza gharama za kununua mbegu hizo pindi wanapohitaji kupanda mazao.
"Tunatekeleza mradi wa RWCC tupo chini ya TGNP sisi tunafanya kilimo cha ikolojia kilimo hiki ni cha asili kabisa ambacho hakitumii kemikali na mbegu zake ni rahisi kupatikana kutokana kwamba tunazitengeneza wenyewe na kuzipanda,jambo hili linamsaidia mwanamke kuepuka kwenda dukani kununua mbegu kila msimu,"amesema.
No comments:
Post a Comment