MZEE MWAKILEMBE, MAST WAINUA SHABA, CHUNYA YAONGOZA MAGEUZI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, October 14, 2025

MZEE MWAKILEMBE, MAST WAINUA SHABA, CHUNYA YAONGOZA MAGEUZI




Na Mwandishi Wetu, Chunya


Mzee Benson Gabriel Mwakilembe (Maarufu Tall) mchimbaji wa miaka mingi na mmiliki mwenza wa Kiwanda cha Kwanza cha Kisasa cha kuchenjua shaba nchini cha Mineral Access Systems Tanzania Ltd (MAST), amesimulia safari yake kutoka kuchimba dhahabu hadi kuwekeza kwenye shaba. Akizungumza na Madini Diary hivi karibuni, ameeleza safari yake ya mafanikio, fursa, changamoto na maono kuhusu mustakabali wa Sekta ya Madini nchini, akisisitiza nafasi ya teknolojia na uwekezaji wa ndani katika kuongeza thamani ya rasilimali za madini nchini.

"Mimi kwenye dhahabu sirudi tena – sasa niko kwenye shaba. Tanzania tuna shaba nyingi kushinda hata nchi ya Zambia! Serikali na wachimbaji waione kama zao kuu la biashara, masoko yapo,’’ anasema Mzee Mwakilembe.

Akizindua kiwand hicho Juni 18, 2025 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alisema kimeiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia kama mzalishaji wa shaba na hivyo kutimiza dhamira ya Serikali kuongeza thamani ya madini kabla ya kusafirishwa nje. Alisema ujenzi wa kiwanda hicho unaonesha dhamira ya Serikali kuongeza thamani ya madini, na uwekezaji wa MAST ni uthibitisho wa mazingira bora ya biashara nchini.

Kwa muktadha huo, katika simulizi yake Mzee Mwakilembe anasema, “katazo la kusafirisha shaba ghafi nje lililotolewa na Serikali ya Awamu ya Tano tuliona limetuumiza sana kibiashara, lakini, ndilo limetufikisha hapa. Awamu ya Sita imeweka mkazo zaidi na sasa ni ajabu, kwa mara ya kwanza, Tanzania tunachenjua shaba hapa na tumeweza kusafirisha copper cement zaidi ya tani 200,’’ anasema Mzee Mwakilembe.

Mbali na leseni za shaba Chunya, Mzee Mwakilembe pia anamiliki leseni Simanjiro, Tunduru, Mpwapwa na Njombe anazolenga kuchimba shaba na kusafirishwa Chunya kwenye kiwanda cha MAST na kueleza kwamba, mpango wa siku za usoni wa kiwanda hicho ni kuchenjua shaba kufikia kiwango cha copper cathode. ( zao la mwisho).

"Madini yamenifaa sana – ninaendesha maisha, nina miradi mingine, sasa nina mabasi mawili ya usafirishaji wa abiria kutoka Tunduru mpaka Mbeya. Nilipotoka na nilipo sasa ni tofauti kabisa… kwa utani anasema, sasa hivi napanda ndege bana, – madini yamenivusha, mimi sikubahatika kusoma!” anasema Mzee Mwakilembe.

Hakuacha kupongeza kuhusu namna viongozi wa Wizara walivyomshika mkono kufika hapo na kusema,’’ kiwanda hiki ni matokeo ya msaada mkubwa kutoka kwa viongozi wa Wizara. Alianza Mhe. Biteko huyu alinifundisha namna ya kupambana na wawekezaji, akaja Waziri Mavunde, kiwanda cha MAST ni nguvu ya Mavunde! Katibu Mkuu Samamba na kijana wangu Rama wa Tume ya Madini, wametupambania sana, na hapa Chunya huyu Afisa Madini na wenzake, wana msaada sana. Natamani uongozi huu uendelee," anasisitiza Mzee Mwakilembe.

Akizungumza siku ya uzinduzi, Mkurugenzi wa MAST, Godfrey Kente alisema lengo la kiwanda ni kuchenjua shaba yenye kiwango cha chini asilimia 0.5 hadi 2 na kuiongeza thamani hadi asilimia 75 kupitia teknolojia ya leaching na cementation.

Kente alisema MAST inatarajia kujenga viwanda vitatu vya shaba Manyara, Ruvuma na Dodoma, ambapo kila kimoja kitatengeneza ajira zaidi ya 500 na kuchangia zaidi ya Dola za Marekani milioni 40 kwa mwaka katika uchumi.

Akizungumza hivi karibuni na Madini Diary, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Kimadini Chunya Mhandisi Laurent Mayala alisema tangu kuanzishwa kwake Aprili 2025, kimezalisha tani 810 za shaba zenye thamani ya Sh10.3 bilioni, na Sh 594 milioni tayari zimetolewa Serikalini.

Kuhusu MAST

MAST ni Kampuni ya Kitanzania, iliyoanzishwa mwaka 2011. Kiwanda hicho ni matokeo ya uwekezaji wa zaidi ya dola milioni 10 za Kimarekani (USD) ikiwa ni uwekezaji wa ubia kati ya Kampuni ya MAST na MCC kutoka New York, Marekani.

Ombi kwa Serikali na taasisi za fedha

"Serikali kupitia STAMICO ikae na taasisi za fedha – wachimbaji wakopeshwe kwa leseni zenye tafiti. Pia, wananchi waelimishwe kuhusu sekta ya madini. Mama ametuletea mashine, lakini ziwafikie wachimbaji wadogo zaidi na gharama za utafiti zipunguzwe," anasisitiza Mzee Mwakilembe.

Vipi kuhusu mageuzi ya Chunya?

"Watu waliokuwa Chunya miaka ya 1980 wakirudi leo watashangaa sana – Chunya imebadilika sana! Haikuwa hivi. Serikali imerahisisha sana shughuli za uchimbaji na biashara ya dhahabu," anasema Mzee Mwakilembe




No comments:

Post a Comment