TPHPA YADHIBITI KWELEAKWELEA KWA KUIMARISHA USALAMA WA MAZAO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, August 5, 2025

TPHPA YADHIBITI KWELEAKWELEA KWA KUIMARISHA USALAMA WA MAZAO

Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imeongeza jitihada katika kudhibiti uvamizi wa visumbufu hatarishi, ikiwemo kweleakwelea, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuboresha kilimo na kutekeleza Agenda 10/30 mpango wa kitaifa unaolenga kuongeza tija na ustawi katika sekta ya kilimo hadi kufikia mwaka 2030.

Kweleakwelea ni ndege vamizi anayeshambulia na kuharibu mazao kama mpunga, alizeti, na nafaka nyingine, hivyo kuhatarisha usalama wa chakula na kupunguza kipato cha wakulima. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, TPHPA kupitia wataalamu wake wa Kanda ya Mashariki imeweka mikakati madhubuti ya ufuatiliaji, tathmini, na udhibiti wa kweleakwelea kabla haijasababisha madhara makubwa mashambani.

Akizungumza katika banda la TPHPA kwenye Maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya Mwl. Julius Nyerere Morogoro, Dkt. Mahudu Sasamalo, Mkuu wa Kanda ya Mashariki, alieleza kuwa TPHPA imeendelea kudhibiti kwa mafanikio maeneo yaliyoathiriwa, ikiwemo Ifakara, Kilosa, Mvomero, na Bagamoyo, ambapo maelfu ya hekta zimeokolewa na mazao ya wakulima kuendelea kustawi.

“Kupitia juhudi hizi za kisayansi na kijamii, tunalenga kuhakikisha wakulima wa Tanzania wanapata mazingira salama ya kilimo bila kutishiwa na visumbufu vya mimea. Hii ni sehemu ya azma ya Serikali ya kuhakikisha kilimo kinakuwa cha kisasa, chenye tija, na chenye mchango mkubwa katika pato la taifa,” alisema Dkt. Sasamalo.

Katika kuendeleza utekelezaji wa Agenda 10/30, inayolenga kuhakikisha kilimo kinachangia angalau asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2030, TPHPA inaendelea kuwekeza katika teknolojia, elimu kwa wakulima, na udhibiti endelevu wa visumbufu mashambani, ikiwemo matumizi ya mbinu rafiki kwa mazingira.

Wananchi na wadau wa kilimo mkoani Morogoro
mnakaribishwa kutembelea banda la TPHPA kwenye Maonesho ya Nanenane ili kujifunza zaidi kuhusu mbinu za kisasa za kulinda afya ya mimea na mchango wa Mamlaka katika kuendeleza kilimo bora na biashara ya mazao nchini

No comments:

Post a Comment