
Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imetoa mafunzo ya Moduli ya Usimamizi wa Mikataba (e-contract) kupitia Mfumo wa NeST, kwa watendaji zaidi ya 300 wa taasisi za umma, Agosti 24 – 29, 2025 jijini Mwanza.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Bw. Elikana Balandya, Katibu Tawala Msaidizi, Bw. Daniel Machunda amesema Serikali imeboresha Mfumo wa NeST ili kuwezesha hatua zaidi za michakato ya ununuzi wa umma kuanzia usajili hadi usimamizi wa mikataba kufanyika kwenye Mfumo huo.
Ameongeza kuwa hatua hiyo itaongeza ufanisi, kupunguza muda na gharama za zabuni; na kutunza mazingira kwa kuondoa matumizi ya karatasi kwenye michakato ya ununuzi nchini.
“Nawasihi washiriki kuhakikisha wanazingatia mafunzo yanayotolewa ili usimamizi wa mikataba ambao awali lilikuwa ni eneo lenye changamoto nyingi hususan za ufuatiliaji, lakini sasa hivi limeboreshwa na kila hatua inafanyika na kuonekana dhahiri kwenye Mfumo,” amesema Bw. Machunda.
Washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kuwa matumizi ya moduli ya usimamizi wa mikataba kupitia Mfumo utawasaidia kuweka kumbukumbu nzuri, kuondo hoja za ukaguzi na kuwa na matokeo bora ya utekelezaji wa mikataba ya ununuzi.
“Kwa siku hizi mbili tulizoanza kupata mafunzo, tayari tumeona kuwa mwisho wa mafunzo haya utakuwa mwanzo mzuri wa kuboresha utekelezaji wa mikataba. Sasa hivi majadiliano [negotiation] na upekuzi wa mikataba [vetting] hadi kusaini mikataba vyote vinafanyika kwenye Mfumo. Tukiwa na uelewa mzuri, hatua hii ya Serikali itasaidia kuimarisha usimamizi wa mikataba ambao utaleta upatikanaji wa thamani ya fedha,” amesema Bw. John Suka, Afisa Ununuzi Mwandamizi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA).

No comments:
Post a Comment