
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Doto Mashaka Biteko amesema kuwa kwa Serikali ya CCM inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya jitihada kubwa ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Wilaya ya Bukombe ikiwa ni pamoja na kutoa fursa za kukuza uchumi wa Wilaya hiyo.
Dkt. Biteko amesema hayo Septemba 27, 2025 wakati wa mkutano wa kampeni katika Kata ya Katente wilayani Bukombe mkoani Geita ikiwa ni sehemu Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Amesema mwaka 2015 Kata ya Katente, Igulwa na Kata zote zilizopo maeneo ya mjini zilikuwa na kiwango duni sana cha maendeleo ikilinganishwa na maendeleo yaliyofikiwa sasa.
Amesema Wilaya ya Bukombe ilikuwa na shule moja ya kidato cha tano na sita, hospitali moja, zahanati nne huku umeme ukiwa katika vijiji saba pekee.
Amesema Serikali ya CCM imekuwa ikifanya jitihada kubwa ya kutekeleza miradi ya maendeleo ili kuboresha maisha ya wananchi wa Wilaya hiyo ambapo sasa inajenga jengo la Ofisi ya Mkuu Wilaya, jengo la halmashauri, soko na stendi ya kisasa.
“ Rais samia ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Ushirombo kwenda Katoro kwa kiwango cha lami ambao unaendelea na ameruhusu watu kuchimba dhahabu katika Pori la Kigosi na sasa vijiji vyote vimepelekewa umeme,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu mbalimbali “ Tunajenga Chuo cha VETA pamoja na Chuo Kikuu vyote hivi vitasaidia kuleta mzunguko wa fedha na kukuza uchumi wetu, watu hawataki maneno wanataka maendeleo na Dkt. Samia amedhamiria kuibadilisha Bukombe,”
Sambamba na hayo, Dkt. Biteko amewahimiza wananchi wa Katente 19,000 waliojiandikisha kupiga kura ifikapo Oktoba 29 wamchague Dkt. Samia kwa nafasi ya Urais, mbunge na diwani wa CCM ili kuendelea kuchochea maendeleo ya Wilaya ya Bukombe.
Akizungumzia katika mkutano wake wa kampeni Kata ya Bulangwa, Dkt. Biteko amesema kuwa Dkt. Samia amesaidia sana kuleta maendeleo katika Kata hiyo na kuwa miaka mitano iliyopita alitoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
“ Hapa Bulangwa tumejenga shule ya watoto wenye mahitaji maalum, tunajenga shule ya sekondari ya kidato cha tano na sita, tunajenga Shule ya Sekondari Bulangwa,” amesema Dkt. Biteko.
Ametaja miradi mingine ya maendeleo iliyojengwa ni ukumbi mkubwa wa mikutano na kituo cha afya.
Aidha, wanatarajia kufikisha umeme katika vitongoji ambavyo havina umeme pamoja na kukamilisha ujenzi wa uwanja wa mpira wa kisasa.
Pamoja na hayo amewaomba wananchi wa Kata hiyo kumpigia kura diwani nyingi diwani anayegombea kwa kuwa kwa miaka mitano iliyopita amefanya kazi nzuri.
“ Kama mbunge ninaridhika mno na kazi inayofanywa na Yusuf kwa sababu anashughulikia maendeleo ya watu. Nawaomba wana Bulangwa tumpe ushirikiano kwa kumpigia kura nyingi ili aendelee kutuletea maendeleo,” amesema Dkt. Biteko.
Ameendelea kusema hakuna maendeleo yanayopatikana bila kupiga kura hivyo amewaomba wananchi wa Bulangwa 15,504 waliojiandikisha kupiga kura wajitokeze Oktoba 29 na wawachague wagombea wa CCM.
Naye, Mgombea wa Udiwani Kata ya Katente, Tabu Ngwahani amesema kata hiyo imenufaika na miradi mingi ya maendeleo kama vile kujenga madarasa katika Shule za Msingi Igulwa, Bomani, Umoja, Bwenda na Katente.
Amesema kuwa wameendelea kupokea fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko, stendi na uwanja wa mpira.
“ Tunaendelea kuboresha barabara, tulipokea shilingi milioni 300 kwa ajili ya hospitali. Pia tulipokea shilingi milioni 900 na tumejenga majengo mengine ikiwemo chumba cha upasuaji,” amesema Nkwandu.
Kwa upande wake, Mgombea wa Udiwani Kata ya Bulangwa, Yusuf Mohammed Yusuf amemshukuru Dkt. Biteko kwa kutoa fedha shilingi milioni 350 kwa ajili ya kujenga Shule ya Kilimahewa.
Amesema kuwa katika Kata hiyo wanatarajia pia kujenga Shule mpya ya Msingi ya Muungano, kujenga barabara pamoja na kusogeza umeme katika Vitongoji vya Kilimahewa na Muungano.







No comments:
Post a Comment