DKT. SAMIA AAHIDI KUMALIZA CHANGAMOTO YA MAJI NA MIUNDOMBINU UYUI, TABORA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, September 11, 2025

DKT. SAMIA AAHIDI KUMALIZA CHANGAMOTO YA MAJI NA MIUNDOMBINU UYUI, TABORA


Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali yake imefanikisha utekelezaji wa miradi 15 ya maji Wilayani Uyui, mkoani Tabora, hatua iliyoongeza upatikanaji wa huduma hiyo kufikia asilimia 67.

Akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo, Alhamisi Septemba 11, 2025, Dkt. Samia alisema Serikali pia inatekeleza mradi wa maji kutoka Ziwa Viktoria utakaosaidia kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji wilayani humo.

Amesema katika mpango huo, Serikali inajenga tanki la kuhifadhi lita milioni moja za maji katika Kata ya Ilolangulu kwa ajili ya kuhudumia wananchi wa kata hiyo pamoja na Kata za Kalola, Isila, Ndono na Mabana.

Aidha, ameahidi kuwa endapo ataendelea kuongoza kwa muhula mwingine wa miaka mitano, atahakikisha miradi ya maji ya Kigwa, Bwawa la Igombe na Kizengi inakamilishwa, akisisitiza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata maji safi, salama na ya uhakika.

Katika sekta ya miundombinu, Dkt. Samia alisema Serikali ya Awamu ya Sita imetenga fedha kwa mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Mto Loya wilayani Uyui, ambapo usanifu na michoro tayari imekamilika.

Alilitaja daraja hilo kuwa suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi wa eneo hilo hasa wakati wa masika.




No comments:

Post a Comment