
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan ametangaza kujengwa kwa Njia ya kusafirisha umeme kutoka Mkoani Ruvuma- Tunduru mpaka Masasi Mkoani Mtwara ili kutoa uhakika wa upatikanaji wa umeme wa kutosha na wa uhakika Mkoani Mtwara kama sehemu ya maandalizi ya ujenzi wa Kongani za Viwanda kwenye Wilaya ya Masasi.
Akizungumza na Maelfu ya wananchi wa Masasi leo Jumanne Septemba 23, 2025 kwenye Viwanja vya Boma kwenye muendelezo wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu, Dkt. Samia amesema ujenzi wa njia hiyo ya umeme, itaambatana na ujenzi wa vituo viwili vya kupooza umeme na kusambaza umeme huo kwa wananchi na katika maeneo ya uwekezaji Mkoani humo.
Aidha katika hatua nyingine Dkt. Samia ameeleza kuhusu jitihada mbalimbali zilizochukuliwa na serikali ya awamu ya sita katika kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, akieleza kuwa ikiwa atapata ridhaa kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, serikali pia itakamilisha ujenzi wa barabara ya Mlivata- Newala- Masasi kwenye kipande cha Mlivata- Mitesa yenye urefu wa Kilomita 100 ambayo itajengwa kwa kiwango cha lami.
Ameahidi pia kuendelea na ujenzi wa barabara za ndani ya Mji wa Masasi zinazojengwa na TARURA, Barabara ambazo zitajengwa kwa viwango vya lami na changarawe.





No comments:
Post a Comment