
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumamosi Septemba 06, 2025 amewaahidi wananchi wa Makambako Mkoani Njombe kuwa kuanzia mwezi Oktoba 2025, Serikali ya awamu ya sita itaanza kujenga vituo vya kuuzia mahindi Mkoani humo kama sehemu ya kutoa fursa ya masoko kwa wakulima wa Mkoa huo.
Dkt. Samia ameyasema hayo wakati wa mkutano wake wa Kampeni kwenye soko kuu la Makambako akiwa njiani kuelekea Mkoani Iringa kuendelea na kampeni yake, akiahidi pia kulifanyia kazi ombi la Mgombea Ubunge wa Jimbo hilo Ndugu Godfrey Chongolo, aliyeomba pia Mji huo kujengewa bandari Kavu kutokana na umuhimu wake wa kuwa kitovu cha biashara kwa Mikoa ya kusini na nchi za Jirani.
"Niwapongeze pia kwasababu tayari chuo cha Mwalimu Nyerere wameshafanya matayarisho ya awali ya ujenzi wa chuo na niseme serikali itatoa fedha yote ili chuo hiki kianze kujengwa na kikamilike na kwa ukweli chuo hiki kipo kwenye mpango wa mabadiliko ya elimu ya juu na fedha yake ipo tayari ni kazi tu ifanyike." Amesema Mgombea Urais huyo.
Dkt. Samia akibainisha kuwa ameingia Makambako kwa ujasiri mkubwa kutokana na yale yaliyotekelezwa Mkoani Njombe kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita pamoja na mipango ya miaka mitano ijayo, ametumia fursa hiyo kuomba kura kwa wananchi wa Makambako, akiwasifu kwa rekodi nzuri za kujitokeza kushiriki kwenye chaguzi za hapo kabla, akiwaomba kujitokeza tena kwa wingi Oktoba 29, 2025 ili kuweza kupiga kura na kuchagua viongozi watakaoweza kusogeza mbele maendeleo ya Jimbo hilo la Makambako.









No comments:
Post a Comment