
Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kufufua na kutafuta masoko ya zao la Chai Wilayani Mufindi Mkoani Iringa, akisema tayari kumeundwa Timu ya Tathmini kufuatilia uwekezaji wa sekta binafsi katika zao hilo ili kuona ikiwa wameshindwa kuendeleza zao hilo ili serikali iingilie kati kwa kuchukua mashamba ya Chai na kuyakabidhi kwa Vyama vya ushirika nchini.
Dkt. Samia ameyaeleza hayo leo Jumamosi wakati akiingia Mkoani Iringa, kwenye Mkutano wa Kampeni Nyororo Wilayani Mufindi, akiahidi kwamba wakulima na wafanyakazi wa Kampuni ya Chai ya Mufindi Tea and coffee Company wanaodai zaidi ya Bilioni 2.7 wataanza kulipwa fedha zao hivi karibuni mara baada ya serikali kufanya naye mazungumzo.
Aidha Dkt. Samia amesema barabara ya Nyororo- Mtwango wilayani Mufindi yenye urefu wa Kilomita 40.4 itaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami sambamba na barabara ya Igowole- Kasanga- Nyigo yenye urefu wa Kilomita 54.5 pamoja na kuahidi kupeleka mashine ya Xray kwenye Hospitali ya Wilaya ya Mufindi Mkoani humo.
Awali Wagombea Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi katika Majimbo ya Mufindi Kaskazini na Mufindi Kusini wamemshukuru Dkt. Samia ambaye pia ni Rais wa Tanzania wa awamu ya sita kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo Wilayani humo ikiwemo utoaji wa zaidi ya Bilioni 40 zilizofanikisha ujenzi wa shule mpya 23 ikiwemo nne za sekondari pamoja na chuo cha ufundi stadi Veta, suala ambalo wanalitaja kama suluhu ya michango mfululizo ambayo wananchi (Wazazi) walikuwa wakitozwa huko nyuma kufanikisha ujenzi wa miundombinu ya elimu Wilayani humo.
Wamemshukuru pia kwa kusogeza huduma ya umeme kwenye maeneo yao ndani ya miaka minne ya uongozi wake suala ambalo limefanikisha Kata zote za Mufindi kuwa na huduma hiyo, Vijiji vyote na vitongoji zaidi ya asilimia 78 vilivyopo Wilayani humo, kando ya ruzuku zilizotolewa kwa wakulima wa mahindi na Chai Wilayani humo hivyo kuwezesha wananchi kununua Mbolea na pembejeo nyingine za kilimo kwa nusu bei.
No comments:
Post a Comment