
Mgombea urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema maendeleo makubwa yaliyotekelezwa katika Manispaa ya Songea ni kielelezo cha utekelezaji wa ilani ya Chama hicho, huku akiahidi kuendeleza kasi ya huduma za kijamii na miundombinu kwa wananchi wote.
Akizungumza na maelfu ya wananchi kwenye Viwanja vya VETA, Songea Mjini leo Jumatatu Septemba 22, 2025, Dkt. Samia amesema katika sekta ya afya, Serikali ya CCM imewezesha ujenzi wa zaidi ya zahanati 10 na vituo vipya vya afya katika maeneo mbalimbali ikiwemo Msamala, Subira, Ndilimalitembo na Mshangano, pamoja na uendelezaji wa Hospitali ya Sanangula.
Aidha, amesema hospitali na vituo vya afya vinaendelezwa kwa kujengewa wodi, maabara na vitengo vya dharura ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora karibu.
Kwa upande wa elimu, Dkt. Samia amesema ujenzi wa madarasa zaidi ya 150, shule mpya za sekondari na msingi, pamoja na hosteli, mabweni na ukarabati wa shule kongwe kama Songea Girls na Songea Boys, ni hatua muhimu ya kuongeza fursa za elimu kwa watoto wa Songea.
Kwenye upande wa barabara na miundombinu, ameeleza kuwa ujenzi wa barabara za lami na changarawe katika maeneo ya Msamala–Mwengemshindo, Souwasa–Mashujaa, pamoja na daraja jipya la Ruhuwiko–Mwengemshindo, umefungua njia za biashara na usafirishaji.
Amesema pia sekta ya biashara na ajira imepewa kipaumbele kupitia ujenzi wa masoko mapya, shopping mall, stendi ya malori Lilambo na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao, hatua ambayo inaleta ajira kwa vijana.
Aidha, Dkt. Samia amesema miradi ya maji safi katika maeneo ya Subira, Sanangula, Sinai, Londoni na Ruhuwiko inaendelea kutekelezwa, lengo likiwa kila kaya kupata maji salama na ya uhakika.
“Wananchi wa Songea wameshuhudia mabadiliko makubwa katika huduma za afya, elimu, barabara na maji. Tunataka kuendeleza kasi hii na kuhakikisha kila familia inanufaika na matunda ya maendeleo,” amesema Dkt. Samia.



No comments:
Post a Comment