
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumatano Septemba 24, 2025 ameweka shada la maua katika Kaburi la aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin William Mkapa, huko Lupaso Wilayani Masasi Mkoani Mtwara.
Hayati Benjamin Mkapa aliongoza awamu ya tatu na ni Rais wa kwanza aliyechaguliwa katika uchaguzi ulioshirikisha vyama vingi vya siasa nchini Tanzania tangu mfumo huo uliporejeshwa mwaka 1992. Aliingia rasmi madarakani Oktoba 1995. Hayati Mkapa alizaliwa Masasi, Mkoani Mtwara tarehe 12 Novemba, 1938 na Kufariki Julai 24, 2020.
Katika Kongamano la Maadhimisho ya Mwaka mmoja tangu kufariki kwa Hayati Mkapa Julai 14, 2021 Rais Samia alinukuliwa akisema kwamba kitabu cha historia ya Tanzania hakiwezi kukamilika bila kuwepo kwa sura nzima yenye kumwelezea Hayati Mkapa na mageuzi mengi aliyoyafanya katika uongozi wake.
“Kitabu cha historia ya Taifa letu hakiwezi kukamilika bila kuwepo kwa sura nzima itakayomwelezea Hayati Mzee Mkapa, sio tu kwasababu alikuwa Rais wetu, lakini pia kutokana na mageuzi makubwa aliyoyafanya kwenye nchi yetu. Alikuwa mtu wa kipekee sana, mara zote ukikutana nae utaondoka umechota maarifa mengi”, alisema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia alisema kwamba Hayati Mkapa ndie aliyeanzisha taasisi nyingi nchini ambazo bado zinaendelea kufanya kazi nzuri mpaka leo. Akizitaja baadhi ya Taasisi hizo ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Taasisi ya Kupambana na Rushwa Tanzania (PCCB) pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF). Taasisi nyingine ni Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKURABITA) na Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS).
Kwa upande wa maendelea ya uchumi wa nchi kwa ujumla Rais Samia alisema kwamba Hayati Mzee Mkapa alifanikiwa kupunguza deni la Taifa kutoka asilimia 143.7 mwaka 1995 hadi asilimia 60.7 mwaka 2005 akichochewa na uwezo wake wa kidiplomasia katika kuzishawishi Taasisi za kifedha za Kimataifa na Nchi wahisani kusamehe madeni kwa kutumia mpango wa Heavily Indebted Poor Countries (HIPC) uliosimamiwa na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF).








No comments:
Post a Comment