Na Mwandishi Wetu
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi, ametoa wito kwa Viongozi, Menejimenti na Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake kubeba malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 kama sehemu ya wajibu wao wa kitaifa ili kuweza kufikia maono yaliyopo kufikia mwaka 2050.
Dkt. Yonazi ametoa wito huo wakati ufunguzi wa Kikao cha Mazingativu ya Menejimenti, Wakuu wa taasisi na Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu na taasisi zake kinachofanyika leo Septemba 25, 2025 Jijini Arusha.
“Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 tayari imeshazinduliwa, Dira hii ni ramani ya mustakabali wa nchi yetu, ikitupa taswira ya nchi ambayo tunaihitaji kuwa nayo katika ndani ya miaka 25 ijayo, ili kufanikisha maono haya kila mmoja wetu anawajibu na anajambo la kulifanya, ni wajibu wetu kujiuliza kwamba nitachangia nini kuhakikisha nchi yangu inafikia maono haya kufikia mwaka 2050” ameeleza Dkt. Yonazi.
Aidha, amebainisha kuwa, kila mmoja mahali pake pa kazi anawajibu kwa kuhakikisha nchi ya Tanzania inakuwa nchi bora na mahali bora pa kuishi kwa kuweka misingi bora ifikapo mwaka 2050.
Akizungumza kuhusu kikao hicho, Dkt. Yonazi amebainisha kuwa, kikao hicho ni sehemu ya utamaduni wa Ofisi ya Waziri Mkuu kutenga muda kila mwaka kwa ajili ya kujitafakari, kujifunza na kujipanga upya kwa lengo la kuboresha utendaji katika kutekeleza majukumu ya Ofisi hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha CPA. Amos Makalla ametoa wito kwa Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuwa wabunifu katika kufikiri na kutekeleza majukumu yao, ili kuweza kutoa huduma zinazokidhi mahitaji na matarajio ya wananchi kwa ufanisi zaidi.
“Dunia ya sasa inabadilika kwa kasi kubwa na changamoto zake zinahitaji mbinu mpya za kuzikabili, ni wajibu wetu kuwa wabunifu katika kufikiri na kutekeleza majukumu yetu, ili tuweze kutoa huduma zinazokidhi mahitaji na matarajio ya wananchi kwa ufanisi zaidi. Hivyo, kubadilika kulingana na wakati ni muhimu ili kuendana na mabadiliko ya kidunia, kitaifa na kijamii, tukizingatia misingi hii, tutakuwa na Ofisi yenye weledi, inayothamini maendeleo endelevu na inayokabiliana na changamoto kwa mafanikio” alisema.
Aidha, Mkuu wa Wilaya huyo amebainisha kuwa “Kwa kuwa jukumu la uratibu, ufuatiliaji na tathmini ya shughuli zote za Serikali lipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, nitumie fursa hii kutoa rai kuwa tuendelee kulitekeleza jukumu hili kwa ufanisi wa hali ya juu. Kila taasisi inapaswa kuonesha matokeo halisi katika maeneo yake ya utekelezaji, tuweke mkazo zaidi katika kuhakikisha kwamba kazi zetu zinajikita kwenye matokeo yanayogusa maisha ya wananchi, badala ya kuishia kwenye michakato au utekelezaji usioonesha matokeo”.
Mbali na hayo Mhe. Mkude ametoa wito wa kushiriki uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kwani Uchaguzi huo ni fursa ya kipekee kushiriki katika kuimarisha misingi ya demokrasia na utawala bora.
“Kila Mtanzania anatakiwa kutimiza haki na wajibu wake wa kikatiba kwa kupiga kura, ili kuchagua viongozi watakaoliongoza Taifa letu katika ngazi zote, aidha, ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha tunadumisha amani, mshikamano na utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi, ili Tanzania iendelee kubaki kuwa mfano bora wa utulivu, mshikamano na demokrasia barani Afrika” ameongeza.
Kikao hicho kinaendelea Jijini Arusha, na mada mbalimbali zitawasilishwa ikiwemo ikiwemo Matumizi ya Akili Unde (AI) mahala pa kazi na mustakabali wa ajira kutokana na maendeleo ya kasi ya sayansi na teknolojia, masuala ya afya ya akili, fursa za uwekezaji kwa watumishi na maandalizi ya maisha baada ya kustaafu, masuala ya itifaki na ustaarabu na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ili kuweza kujiimarisha katika nyanja mbalimbali kitaaluma, kimaisha na kiutumishi.
No comments:
Post a Comment