Maabara za Madini Zahimizwa Kutumia Crucibles Zilizotengenezwa GST ili Kuongeza Tija - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, September 25, 2025

Maabara za Madini Zahimizwa Kutumia Crucibles Zilizotengenezwa GST ili Kuongeza Tija




Na Mwandishi, Geita


Maabara zinazojishughulisha na uchunguzi wa sampuli za madini nchini zimehimizwa kutumia vikombe (crucibles) vya kuyeyushia sampuli zenye madini ya dhahabu vinavyotengenezwa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili kuongeza tija kwenye uchunguzi wa madini ya dhahabu kwa njia ya tanuru (fire assay).

Hayo yamesemwa leo, tarehe 25 Septemba 2025, na Bw. Gideon Nshange, Fundi Sanifu Mkuu – GST, wakati akizungumza na wadau waliotembelea banda la GST katika Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili, Manispaa ya Geita.

Akielezea sifa za vikombe hivyo, Bw. Nshange alisema vina ubora wa hali ya juu, unaochangiwa na uwezo wake wa kuhimili joto kali hadi nyuzi joto 1400.

Aidha, vikombe hivyo vinaokoa gharama za uendeshaji kwani vina uwezo wa kuyeyushia sampuli zenye madini ya dhahabu kwa zaidi ya mizunguko mitatu.
Mbali na sifa hizo, vikombe hivyo vinauzwa kwa bei nafuu.

Bw. Nshange ameongeza kuwa kutokana na ubora huo, mwitikio wa wateja umekuwa mkubwa. Wale waliovijaribu hawakujuta, na sasa wamekuwa wateja wa kudumu.

GST imekuwa ikizalisha vikombe hivyo kwa matumizi ya ndani na kwa wateja wa nje kwa takribani miaka 15 sasa.

Aidha, vikombe vinavyozalishwa na GST vinapatikana katika ujazo tofauti (D50 na D65).




No comments:

Post a Comment