MAVUNDE AANZA RASMI KAMPENI JIMBO LA MTUMBA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, September 3, 2025

MAVUNDE AANZA RASMI KAMPENI JIMBO LA MTUMBA



Na Okuly Julius, Dodoma


Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mtumba kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Anthony Mavunde, leo ameanza rasmi kampeni zake kwa kishindo katika mkutano uliofanyika Kata ya Ipagala, Jijini Dodoma.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, John Mongela, ambaye alimtambulisha rasmi Mavunde pamoja na wagombea udiwani 20 wa kata na viti maalum.

Katika hotuba yake, Mongela aliwataka wanachama wa CCM kutobweteka, akisisitiza kuwa hata maeneo ambayo chama kimekosa wapinzani bado ni muhimu kujitokeza kupiga kura za “ndiyo” kwa mujibu wa sheria mpya ya uchaguzi.

Kwa upande wake, Mavunde aliwaomba wananchi wa Mtumba kumpa ridhaa ya kuendelea kulitumikia jimbo hilo, akiahidi kuendeleza kasi ya maendeleo na kuvunja rekodi za watangulizi wake. Alitaja kipaumbele chake kuwa ni kuboresha huduma za afya, elimu, maji safi na salama, pamoja na kuimarisha fursa za ajira kwa vijana.

“Jimbo letu lina fursa kubwa, jukumu langu ni kuhakikisha kila mmoja wenu ananufaika na matunda ya Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema Mavunde huku akishangiliwa na wananchi.

Aidha, alitaja vipaumbele maalum vitatu atakavyoshughulikia mara baada ya kuchaguliwa kuwa ni kuboresha miundombinu ya barabara za ndani, kumaliza tatizo la mgawo wa maji kwa kuchimba visima vitano, na kuimarisha elimu kwa kununua mashine za fotokopi kwa shule zenye changamoto ya uchapishaji wa mitihani.

Mbali na hayo, ameahidi kujenga shule mpya zikiwemo zenye ghorofa, na kuhakikisha migogoro ya ardhi katika jimbo hilo inamalizwa ili wananchi waishi kwa amani na utulivu.

Kwa mujibu wa taarifa za uchaguzi, Jimbo la Mtumba lina jumla ya kata 20, ambapo wagombea wa CCM katika kata 14 hawana wapinzani, huku kata 6 zikishuhudia ushindani kutoka kwa vyama vingine.



No comments:

Post a Comment