NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimezindua rasmi Bonanza la Michezo kama sehemu ya shamrashamra za kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.
Bonanza hilo lililofanyika Septemba 22, 2025, katika viwanja vya chuo hicho jijini Dar es Salaam, limehusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa wavu, mpira wa kikapu, kuvutana kamba, kufukuza kuku, kukimbia magunia pamoja na riadha.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa Chuo cha NIT, Dkt. Prosper Mgaya, amesema lengo la bonanza hilo ni kuimarisha mshikamano, ushirikiano na afya za washiriki, ili kuongeza ari ya utendaji miongoni mwa watumishi na jamii ya NIT kwa ujumla.
“Nipende kuwahakikishia kuwa mapendekezo yaliyotolewa na kamati ya maandalizi, ikiwemo ukarabati wa miundombinu ya michezo chuoni, yamepokelewa kwa uzito mkubwa na yatazingatiwa katika mipango ya maendeleo ya chuo chetu,” amesema Dkt. Mgaya.
Ameongeza kuwa bonanza hilo limekuwa chachu ya kuhamasisha watumishi kushiriki ratiba ya mazoezi ya kila wiki kwa ajili ya ustawi wa afya zao, hatua iliyosababisha chuo kuandaa vifaa na nyenzo mbalimbali za michezo ili washiriki wote wapate nafasi ya kufanya mazoezi kwa ufanisi.
Aidha, Dkt. Mgaya ameahidi kuchangia kiasi cha Shilingi milioni mbili kwa ajili ya bonanza hilo pamoja na maandalizi ya sherehe za kufunga maadhimisho ya miaka 50 ya NIT.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bonanza, Cornelio Swai, amesema licha ya changamoto za mwingiliano wa ratiba na ufinyu wa bajeti, bonanza limefanikiwa kuvutia ushiriki kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Naye Makamu wa Chuo, Dkt. John John, amebainisha kuwa timu zote zimejiandaa kikamilifu kushiriki michezo hiyo kwa nidhamu na mshikamano, hatua itakayoongeza hamasa na mshikikano miongoni mwa washiriki.
No comments:
Post a Comment