
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama tawala, Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumanne Septemba 23, 2025 ataendelea na ziara yake ya Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, zamu hii akimalizia Nakapanya Mkoani Ruvuma, njiani kuingia kwenye Mkoa wa Mtwara, akifanya mikutano kwenye Wilaya za Nanyumbu na Masasi Mkoani humo.
Uchaguzi Mkuu wa Tanzania unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba na Dkt. Samia ameendelea kuchanja mbuga kwenye Mikoa mbalimbali Ya Tanzania, huku pia Mgombea wake mwenza Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwa kwenye Mikoa ya Nyanda za juu Kusini Magharibi mwa Tanzania, wote wakinadi sera na Ilani za Chama Cha Mapinduzi na kueleza mafanikio makubwa na rekodi nyingi njema zilizowekwa na Dkt. Samia katika kuwatumikia wananchi kwa miaka minne na nusu iliyopita.
Katika Ilani wanayoinadi, pamoja na mengine mengi, CCM inayoongozwa na Dkt. Samia kwa Mkoa wa Mtwara wameahidi kwamba watatekeleza mikakati ya kudhibiti ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto, wasichana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu, kuimarisha malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto pamoja na kuhakikisha mifumo ya malezi inazingatia uwajibikaji na utunzaji wa familia katika jamii pamoja na kuimarisha huduma za ustawi kwa wazee ikiwemo huduma za afya, matunzo na ushirikishwaji katika maamuzi na shughuli mbalimbali za maendeleo.
Aidha wameahidi pia kuongeza upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya kutoka asilimia 93 hadi asilimia 100, kuongeza idadi ya majengo ya huduma za dharura katika Hospitali za Wilaya kutoka 5 hadi 9, kuongeza idadi ya Zahanati kutoka 350 hadi 400, kuongeza idadi ya Vituo vya afya kutoka 66 hadi 83 pamoja na kupunguza udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano na kuongeza huduma za lishe kwa makundi yaliyoathirika zaidi ikiwa ni pamoja na watoto, wajawazito na Vijana rika balehe.
Kwenye Ilani wameahidi pia kuongeza upatikanaji wa mbegu bora na kwa bei nafuu kutoka tani tano hadi 30, kuongeza upatikanaji wa mbolea za ruzuku kwa wakulima kutoka tani 3, 233.2 hadi tani 13, 000, kuongeza upatikanaji wa viuatilifu kutoka Lita 13, 670 hadi lita 21, 382, kuanzisha vituo 4 vya kukodisha zana za kilimo, kuongeza skimu za umwagiliaji kutoka 25 hadi 30, kuongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 5, 324 hadi 8,000 pamoja na kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara na kuimarisha huduma za ugani kwa kutoa vitendea kazi kwa maafisa ugani ikiwemo pikipiki 1200, vishkwambi na vipima udongo takribani 20.
No comments:
Post a Comment