
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule amekemea vikali vitendo vya wizi wa Miundombinu ya Majitaka, hasa mifuniko ya chuma ya chemba za majitaka katika Jiji la Dodoma,vitendo vilivyoibuka na kushamiri kwa kasi siku za hivi karibuni.
Mhe. Mkuu wa Mkoa huo, amekemea vitendo hivyo wakati wa ziara yake akiambatana na Kamati ya Usalama Mkoa aliyoifanya Septemba 19, 2025 katika maeneo mbalimbali ya Mjini Kati Dodoma.

Mhe. Senyamule ameonyesha kukerwa na tabia hiyo inayofanywa na baadhi ya watu wasio na woga wa mali za serikali, na kwamba serikali itachukua hatua kali za kisheria, ikiwa ni pamoja na kuwapeleka mahakamani kwa kuwa vitendo wanavyofanya ni uhujumu uchumi.
Mhe. Senyamule ameahidi kupambana na kadhia hiyo ndani ya Mkoa kwa kuviagiza vyombo vya dola kuanza kazi kwa kuwabaini wahalifu hao pamoja na wanunuzi kwani makundi yote hayo yanachofanya ni uhalifu, uhujumu uchumi na kuhatarisha usalama wa raia wengine.

Awali akitoa taarifa kwa Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma juu ya changamoto hiyo ya wizi wa mifuniko ya chuma ya chemba za majitaka katika maeneo ya katikati ya Jiji la Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph amesema hadi kufikia mwezi Agosti, 2025 mifuniko takribani 61 imeibiwa ikiwa ni hasara kwa serikali ya shilingi Milioni 91.



No comments:
Post a Comment