
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kufanya uwekezaji wa kutosha ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma Bora za magonjwa ya moyo na mishipa.
Amesema kuwa uwekezaji huo unaenda sambamba na dhamira ya kuendelea kupunguza gharama za matibabu hayo kwa kwenda nje ya nchi hivyo kusaidia kuokoa maisha ya Watanzania.
Amesema hayo leo Jumapili (Septemba 28, 2025) alipokuwa mgeni rasmi katika mbio za hisani za Saifee Marathon zilizoanzia na kuishia katika viwanja vya green park Oysterbay, jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza katika ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kutoa huduma za uchunguzi ikiwemo ECHO, ECG, Ultrasound na Holter.
Amesema kuwa takwimu za Shirika la Afya duniani zinaonesha kuwa takribani asilimia 71 ya vifo vyote duniani vinasababishwa na magonjwa yasiyoambukiza. "Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 4.9 wenye umri wa kuanzia miaka 30 hadi 79 wanamatatizo ya moyo na mishipa ya damu".
"Ndugu wananchi nendeni mkafanye uchunguzi ili muwe na uhakika wa afya zenu, zamani huduma hizi ililazimu kusafiri kwenda kwenye nchi kama India, Uingereza na Ujerumani lakini kwasasa tiba hizi ziko hapahapa nchini".
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa kushirikiana na wadau wote wa afya kwenye kutoa elimu ya jamii kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kwa kuwa yamethibitishwa kwamba ni hatari.
"Sisi wananchi tunaowajibu wa kuhakikisha tunafanya uchunguzi wa afya zetu mara kwa mara kwani kugundua tatizo mapema huwezesha matibabu kwa wakati na kuokoa maisha".
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji WA Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza sera ya afya ya mwaka 2007 ikilenga kuboresha huduma za magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo shinikizo la juu la damu " Huduma hizi zinatolewa katika ngazi zote za vituo vya huduma za afya".
Ameongeza kuwa, nchini Tanzania takwimu zinaonesha kuwepo kwa ongezeko la wagonjwa wa shinikizo la damu kutoka wagonjwa milioni 1.73 mwaka 2023/2024 hadi wagonjwa milioni 1.77 mwaka 2024/2025 Sawa na ongezeko la asilimia 98.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Saifee Murtaza Alibhai amesema kuwa dhamira ya mbio hizo hazijaishia kukimbia pekee, bali zinalenga kuelimisha jamii na kusisitiza kinga ya afya.
Ameongeza kuwa mikakati ya hospitali hiyo inaunga mkono Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 inayosisitiza maendeleo ya watu. "Tunajivunia na kumuunga Mkono Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ukuaji wa sekta ya afya nchini".
Lengo la marathon hizo ni kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuchukua hatua za kujikinga na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu kwa kutoa elimu ya afya kwa wananchi kuhusu mtindo bora wa maisha.
Lengo lingine ni kuimarisha uchunguzi wa mapema wa magonjwa yasiyoambukiza, pamoja na kuhimiza ushirikiano wa wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.









No comments:
Post a Comment