
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuwa katika kipindi cha Miaka mitano Ijayo ikiwa wananchi watampa ridhaa ya kuunda serikali, serikali yake itajengwa uwanja mkubwa wa michezo Msoga, Chalinze Mkoani Pwani.
"Hii ni shukrani yetu kwa utumishi wa Rais wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, mengi tumeyapa majina Kikwete lakini sio Msoga, hapa hatukufanya kitu kwahiyo uwanja ule tutauweka Msoga kuonesha shukrani yetu kwa Rais wa awamu ya nne." Amesema Dkt. Samia.
Dkt. Samia ametoa taarifa hiyo leo Jumapili Septemba 28, 2025 wakati wa Kampeni zake kwenye eneo la Msoga Junction Mkoani humo akiwa Njiani kuelekea Mkoani Tanga, akiahidi pia kuendelea kusogeza huduma za kijamii karibu zaidi na wananchi pamoja na kuendelea na uhakiki wa madai ya fidia kwa baadhi ya wananchi wa Msata waliopisha miradi ya maendeleo kwenye eneo hilo Mkoani Pwani.
No comments:
Post a Comment