
Na OKULY JULIUS, OKULY BLOG, DODOMA
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, amesema kuwa kuzinduliwa kwa kamati za usimamizi na utekelezaji wa Mkakati wa Muda wa Kati wa Mapato kutasaidia kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuendeleza miradi ya maendeleo bila kutegemea wafadhili wa nje.
Dkt. Mwamba alitoa kauli hiyo leo, Septemba 18, 2025 jijini Dodoma, wakati wa hafla ya uzinduzi wa kamati hizo ambazo ni Kamati Tendaji na Kamati ya Wataalam zitakazoshirikiana katika utekelezaji wa mkakati huo.
“Kutekelezwa kwa mkakati huu kutaboresha usimamizi wa mapato ya Serikali na kuhakikisha tunakuwa na bajeti endelevu itakayowezesha Serikali kuongeza kasi ya utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi kwa kutumia mapato ya ndani. Natambua kuwa Kamati Tendaji imeundwa na wataalamu wenye uzoefu katika masuala ya uchumi, kodi na fedha kutoka Serikalini na sekta binafsi, sambamba na Kamati ya Wataalam watakaoshirikiana kuhakikisha mkakati huu unaleta matokeo chanya,” alisema Dkt. Mwamba.

Ameongeza kuwa mkakati huo umeainisha maboresho ya kimfumo na hatua mbalimbali ambazo Serikali imeendelea kuzitekeleza ili kuongeza mapato ya ndani.
Hatua hizo zimegawanyika katika makundi matatu:
Mapendekezo ya maboresho ya Sera Mapendekezo ya maboresho ya usimamizi wa ukusanyaji wa mapato
Maboresho ya sheria
Katika eneo la usimamizi wa kodi, mkakati unapendekeza:
Kuandaliwa kwa Sera ya Taifa ya Kodi itakayotoa mwongozo wa uboreshaji wa sera za kodi,Kuboresha mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato,Kuimarisha utii na uhiari wa ulipaji kodi,Kuboresha usajili wa walipakodi,Kuimarisha usimamizi wa misamaha ya kodi,
Kuboresha marejesho ya kodi na viwango vya kodi,
Kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato kutoka katika uchumi wa kidijitali,Kuboresha usimamizi wa mapato ya forodha.
Kwa upande wake, Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera, Dkt. Johnson Nyella, alisema kuwa jukumu kuu la Kamati Tendaji na Kamati ya Wataalam ni kuhakikisha msingi imara wa ukusanyaji wa mapato unawekwa, mianya ya ukwepaji kodi inazibwa, na Taifa linaweza kufanikisha kujitegemea kiuchumi.
Mkakati huu unatarajiwa kuanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo utekelezaji wake unahitaji mshikamano wa Serikali na watendaji wake ili kuhakikisha msingi wa mapato endelevu unaimarika na kuleta maendeleo kwa Watanzania.
Kamati hizo zitakuwa zikikutana mara kwa mara kwa ajili ya kufanya tathmini ya utekelezaji wa mkakati huo.

No comments:
Post a Comment