
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo ameahidi kuendeleza mapinduzi ya kidigitali katika sekta ya elimu kwa kushirikiana na Kampuni ya eee Austria. Prof. Nombo amesema Serikali iko tayari kutumia teknolojia za TEHAMA katika ngazi zote za elimu ili kuhakikisha walimu na wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunza na kufundisha.
Katika mazungumzo yake na Bi. Theresa Wutz, Afisa Mkuu Muidhinishaji wa Miradi wa Kampuni ya eee Austria, Prof. Nombo alipongeza hatua ya Austria kupitia UniCredit –Bank of Austria kuendelea kufadhili Mradi wa Elimu Kidigitali Zanzibari na kueleza kuwa msaada huo utafungua fursa za kupanua matumizi ya TEHAMA hadi shule na vyuo vya Tanzania Bara.
Prof. Nombo alisisitiza kuwa ushirikiano huu ni sehemu ya utekelezaji wa sera za Serikali za kukuza ubora wa elimu kupitia teknolojia na ni mfano hai wa diplomasia ya uchumi inavyoweza kubadilisha maisha ya wananchi, hivyo kukamilika kwa awamu za mradi huo kutaiwezesha Tanzania kuwa na mifumo madhubuti ya kidigitali, miundombinu imara, na rasilimali watu yenye ujuzi wa kisasa katika elimu.



No comments:
Post a Comment