
Katika kuhakikisha usalama na uendelevu wa matumizi ya teknolojia ya nyuklia, Tanzania imeanza kuandaa rasilimali watu wa Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia katika vyuo vya ndani na nje ya nchi Ili kujenga uwezo wa kitaifa na kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje ya nchi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, ameeleza hayo Vienna, Austria 17 Septemba 2025
wakati wa kikao maalum na Mkurugenzi wa Divisheni ya Afrika wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA), Dkt. Gashaw Gebeyehu Wolde, kando ya Mkutano Mkuu wa 69 wa IAEA.
Katika kikao hicho, viongozi hao wamejadili maendeleo ya matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia katika sekta za Afya, Kilimo, Maji na Nishati, sambamba na maandalizi ya wataalamu wa ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya nyuklia.
Prof. Nombo amesema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na IAEA umeleta tija kubwa katika sekta ya afya kupitia matibabu ya saratani kwa mionzi, katika kilimo kupitia tafiti za mbegu bora, na katika maandalizi ya matumizi ya nishati safi ya nyuklia.
Dkt. Gashaw Gebeyehu Wolde amepongeza juhudi za Tanzania na kubainisha kuwa ni mshirika muhimu wa IAEA katika ukanda wa Afrika. Ameahidi kuendeleza ushirikiano wa karibu katika miradi ya nyuklia na kuongeza fursa za mafunzo kwa wataalamu wa sekta ya sayansi na teknolojia ya nyuklia, hususan katika vifaa tiba.
Prof. Nombo anaongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 69 wa IAEA unaoendelea Vienna, Austria.
No comments:
Post a Comment