DKT. SAMIA KUTUA NUNGWI, MUENDELEZO WA KAMPENI ZAKE ZANZIBAR - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, September 18, 2025

DKT. SAMIA KUTUA NUNGWI, MUENDELEZO WA KAMPENI ZAKE ZANZIBAR


Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Alhamisi Septemba 18, 2025 anaingia Nungwi, Kaskazini Unguja Visiwani Zanzibar kwenye siku yake ya pili ya Kampeni Visiwani humo kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Jana Septemba 17, 2025 akiwa kwenye Viwanja vya Kajengwa Jimbo la Makunduchi, Dkt. Samia ameutaja muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuendelea kuimarika na hivyo kuchangia maendeleo ya Kijamii, biashara na uchumi, huku ukilinda uhuru na mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, akisema serikali yake imeendelea kudumisha umoja, amani na utulivu nchini, tunu ambazo zimejenga Taifa na kuipa Tanzania utambulisho wa pekee Kimataifa.

Dkt. Samia pia alieleza kuhusu mpango wake wa kujenga Kituo cha kumbukumbu na nyaraka za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ili kiwe rejeo kwa vijana na wageni wanaotaka kujifunza historia, maana na maendeleo ya Muungano huo wa kupigiwa mfano duniani, kati ya Muungano uliodumu zaidi kwasasa.

Kuelekea uchaguzi Mkuu, ilani anayoinadi Dkt. Samia pamoja na mambo mengine imeeleza Vipaumbele vyake kwa Zanzibar kuwa ni pamoja na kuendelea kuwaunganisha Wazanzibar na kudumisha umoja, amani, utulivu, ushirikiano, maridhiano na uvumilivu, kujenga uchumi imara utakaozingatia usawa na kunufaisha maeneo yote ya Zanzibar pamoja na kuimarisha upatikanaji wa ajira kwa vijana kwa kuzalisha angalau ajira 350, 000 kwenye sekta rasmi na isiyo rasmi ifikapo mwaka 2030.

CCM pia imeahidi kuhakikisha uhakika wa chakula kwa kuanzisha hifadhi ya Taifa cha chakula na kuongeza uzalishaji wa ndani, kuimarisha uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kwa kuendelea kutoa mikopo na kushajihisha matumizi ya teknolojia na mafunzo ya umahiri, kuanzisha makazi bora na upendezeshaji wa miji, kuweka vivutio maalumu vya kushajihisha uwekezaji wa sekta binafsi katika sekta kuu za uchumi Zanzibar pamoja na kuimarisha hifadhi ya jamii kwa wote.

Ilani aliyonayo Mgombea Dkt. Samia pia imetaja mazingatio maalumu kuhusu Zanzibar, ikisema maeneo makuu ya utekelezaji yatakuwa ni pamoja na kuchochea mapinduzi ya uchumi wa kisasa na endelevu, kuchochea mapinduzi ya kidigitali, kukuza huduma za habari na mawasiliano, kuboresha maisha ya watu na ustawi wa jamii pamoja na kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji.

No comments:

Post a Comment