
Na Mwandishi Wetu, Geita
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Geita inahudumia mtandao wa barabara upatao Km. 7274 na kati ya hizo Km. 564 ya barabara zinazohudumia maeneo ya madini.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa TARURA Mkoa wa Geita Mhandisi David Msechu wakati akiongea na waandishi wa habari katika Maonesho ya Nane ya Madini yanayoendelea Mkoani hapa.
Amesema katika mtandao huo asilimia 60 ya barabara zinapitika hivyo maonesho hayo licha ya kutoa elimu kwa umma,wanashiriki kikamilifu kuhakikisha wanaendeleza ukuaji wa uchumi pamoja na kuendeleza huduma za jamii kwa kuhudumia barabara zinazoelekea maeneo ya migodini.
Aidha, Mhandisi Msechu amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na 2025/2026 wametenga kiasi cha shilingi milioni 580 kwa ajili ya kukamilisha Km. 210 zikiwemo barabara zinazoelekea migodini.
Kwa upande mwingine Mhandisi Msechu amesema TARURA Geita wana Maabara ya kisasa ambayo inapima ubora wa vifaa vya ujenzi wa miundombinu ya barabara pamoja na miundombinu mingine inayotekelezwa na Taasisi nyingine zikiwemo TANESCO, Tume ya Umwagiliaji pamoja RUWASA ambayo inatumia maabara hiyo kutekeleza miradi yao kwa ubora unaohitajika.
Naye, Mhandisi wa Miradi kutoka TARURA Makao Makuu Faizer Mbange amesema wanatumia maonesho hayo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya barabara ikiwemo kutokupitisha wanyama kwenye barabara, kulinda na kutunza barabara, kuepuka kulima kandokando ya barabara pamoja na kutopitisha mizigo mizito kwenye barabara.
Amesema wananchi wengi waliotembelea banda la TARURA baadhi yao walikuwa na changamoto ya kutoelewa masuala ya fidia hivyo wameweza kutoa elimu hiyo pia.
“TARURA inatekeleza miradi kwa fedha za ndani pamoja na ile ya fedha za ufadhili hivyo ipo baadhi ya miradi ambayo ina fidia”.
Ameongeza kusema kwamba TARURA pia imeweza kutoa elimu ya uanzishaji wa vikundi kazi kwa ajili ya matengenezo madogo madogo ya barabara ambapo vikundi hivyo huhusika pia katika ulinzi wa barabara hizo.




No comments:
Post a Comment