TARURA GEITA YAZIDI KUPAA: MWENGE WA UHURU WAWEKA JIWE LA MSINGI BARABARA YA KASCO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, September 3, 2025

TARURA GEITA YAZIDI KUPAA: MWENGE WA UHURU WAWEKA JIWE LA MSINGI BARABARA YA KASCO


Na Mwandishi Wetu, Geita


Mkimbiza Mwenge Kitaifa 2025 Ndugu Ismail Ali Ussi amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Geita pamoja na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoani humo muda mfupi baada ya kuweka jiwe la msingi mradi wa barabara ya Kasco.

Amesema kilio cha wananchi wa Geita kuhusu changamoto za miundombinu kinaendelea kupata majibu ya vitendo. Leo, katika eneo la Kasco hadi Shule ya Sekondari Nyanza, Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025 umeweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa barabara ya lami nyepesi yenye urefu wa kilomita 1.32, hatua inayoongeza chachu ya maendeleo kwa wakazi wa Manispaa ya Geita.
Mradi huo unaotekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Geita kupitia fedha za mapato ya ndani, unasimamiwa na TARURA Geita huku mkandarasi akiwa ni kampuni ya Evax Construction Ltd ya Mureba. Kwa mujibu wa mkataba namba 63CC1/2924/2025/W/03, gharama ya ujenzi ni shilingi 999,950,000.00.

Kwa mujibu wa taarifa ya Meneja wa TARURA Wilaya ya Geita, Mhandisi Bahati Subeya, mradi huo ulianza Machi 7, 2025 na unatarajiwa kukamilika Septemba 8, 2025. Hadi sasa umefikia asilimia 95 ya utekelezaji, ambapo zaidi ya shilingi milioni 754 zimeshalipwa.

Mhandisi Subeya amesema mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi, yakiwemo kupunguza adha ya usafiri wakati wote wa mwaka, kuchochea biashara na kuboresha mandhari ya mji.
 
Baada ya kukagua mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ndg. Ismail Ali Ussi, alisifu ubora wa utekelezaji akisema hakuna chembe ya ubabaishaji.

 “Nimetembea mikoa 24, huu ni mkoa wa 25. Sikuwahi kuona miradi ya kiwango cha juu kama hii inayotekelezwa na TARURA. Jana nilizindua barabara ya Nzera, leo Kasco, yote kwa ubora wa hali ya juu. Hakuna harufu ya ufisadi, hakuna ubabaishaji – kazi hii inastahili saluti,” amesema Ussi huku akishangiliwa na wananchi.
 
Aliongeza kuwa miradi inayotekelezwa chini ya usimamizi wa TARURA ni ushahidi kuwa kodi zinazotozwa kwa wananchi zinatendewa haki. 

Pia aliipongeza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Geita kwa kuendelea kulinda amani, jambo lililompa faraja kubwa katika ziara hiyo ya Kitaifa.

No comments:

Post a Comment