VIWANDA VITOKANAVYO NA MADINI YA VIWANDANI VYABADILI MKOA WA TANGA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, September 10, 2025

VIWANDA VITOKANAVYO NA MADINI YA VIWANDANI VYABADILI MKOA WA TANGA



Na Mwandishi Wetu, Tanga,


Sekta ya Madini inaendelea kuandika sura mpya ya maendeleo katika Mkoa wa Tanga, huku viwanda vinavyotokana na madini ya viwandani vikibadilisha taswira ya uchumi, ajira na maendeleo endelevu mkoani humo.

Akizungumza na Madini Diary Septemba 09, 2025, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga, Mhandisi Laurent Bujashi, alisema uwekezaji mkubwa katika ujenzi na uendeshaji wa viwanda vya kuchakata madini kama Chokaa, Madini Tembo, Kaolin, Chumvi, Graphite, Dolomite na Feldspar umeongeza thamani ya rasilimali zilizopo na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.

“Viwanda hivi vimekuwa kichocheo cha maendeleo, si tu kwa kuongeza mapato ya Serikali kupitia tozo na kodi, bali pia kwa kuleta ajira kwa vijana na kuchochea biashara ndogondogo zinazozunguka shughuli za viwanda,” alisema Mhandisi Bujashi.

Kwa mujibu Afisa Madini Mkazi huyo, Mkoa wa Tanga hivi sasa unaonekana kama kitovu cha viwanda vitokanavyo na madini ya viwandani, hatua inayounga mkono ajenda ya kitaifa ya Tanzania ya kujenga uchumi shindani kupitia sekta ya madini na viwanda sambamba na sekta ya madini kufungamanisha na sekta nyingine kama kilimo.

Aidha, aliongeza kuwa ujenzi wa viwanda hivi unaleta fursa mpya za uwekezaji, usafirishaji wa bidhaa ndani na nje ya nchi, pamoja na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine kama kilimo, maji na ujenzi.

Kwa upande wa ukusanyaji maduhuli, Mhandisi Bujashi alifafanua kuwa Mkoa wa Tanga umekusanya asilimia 25 ya lengo la Mwaka wa Fedha 2025/26 la shilingi bilioni 11, ndani ya kipindi cha miezi miwili tu ya Julai na Agosti. Hatua ambayo ni kielelezo cha namna sekta ya madini inavyochangia kwa ufanisi mapato ya Serikali na maendeleo ya kijamii.

Pia, Mhandisi Bujashi alitumia nafasi hiyo kuwahimiza wananchi na wachimbaji wadogo wa Tanga kutumia fursa hiyo kwa kushiriki kikamilifu katika shughuli zinazohusiana na viwanda, ikiwemo usambazaji wa malighafi, huduma za usafiri na ujuzi wa kitaalamu.

Kwa upande wake, Meneja wa Uendeshaji wa Kiwanda cha Newport Minerals Ltd, Geofrey Mramba alisema Kiwanda hicho kinatengeneza malighafi za kuzalishia rangi, chokaa na bidhaa zingine zinazotumika katika sekta za viwanda na ujenzi.

“Uwepo wa madini haya ndiyo ilikuwa sababu kubwa kuchagua kuwekeza hapa Tanga mjini, urahisi wa upatikanaji wa malighali na masoko” alisema Mramba.

Mramba aliongeza kuwa, kupitia uwekezaji huo wakazi wanaozunguka mradi wameajiriwa kupitia ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kama utoaji wa huduma za usafiri, chakula na nyinginezo ambazo zimesaidia kuongeza mnyororo wa thamani na mzunguko wa fedha katika mkoa huo.








No comments:

Post a Comment