
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Jenifa Christian Omolo, akitoa hutuba yake kwa Wahitimu wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), wakati wa mahafali ya 47 ya Bodi hiyo, yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC - Mbweni, jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya Wahitimu pamoja na wageni waalikwa wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi kwenye mahafali ya 47 ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC-Mbweni, jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Jenifa Christian Omolo, akiwatunuku wahitimu kwenye mahafali ya 47 ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC-Mbweni, jijini Dar es Salaam.

Wahitimu wakishangilia mara baada ya kutunukiwa CPA wakati wa mahafali ya 47 ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC-Mbweni, jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Jenifa Christian Omolo, akitoa cheti kwa Mhitimu Kelvin Sanula kwa kufanya vizuri katika mitihani ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), wakati wa mahafali ya 47 ya Bodi hiyo, yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC-Mbweni, jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Jenifa Christian Omolo, akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) ngazi mbalimbali, wakati wa mahafali ya 47 ya Bodi hiyo, yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC-Mbweni, jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Jenifa Christian Omolo, akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) wakati wa mahafali ya 47 ya Bodi hiyo, yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC-Mbweni, jijini Dar es Salaam.

Wahitimu wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) wakiwa kwenye maandamano ya kitaaluma wakati wa mahafali ya 47 ya Bodi hiyo yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC-Mbweni, jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA. Prof. Sylvia S. Temu akizungumza kuhusu mafanikio mbalimbali ambayo Bodi imeyapata toka kuanzishwa kwake, wakati wa mahafali ya 47 ya Bodi hiyo, yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC-Mbweni, jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Pius A. Maneno, akizungumza wakati wa mahafali ya 47 ya Bodi hiyo, yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC-Mbweni, jijini Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dar es Salaam)
Na. Saidina Msangi, WF, Dar es Salaam.
Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) imehimizwa kuendelea kusisitiza wanachama wake umuhimu wa kuzingatia misingi ya uaminifu na uadilifu katika kazi zao za kila siku ili kuondoa mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali na kuongeza tija na ufanisi katika maendeleo ya nchi.
Rai hiyo ilitolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Natu El-maamry Mwamba, wakati wa Mahafali ya 47 ya Bodi hiyo yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC-Mbweni, Dar es Salaam.
Alisema NBAA inatakiwa kuisaidia Serikali katika kuhakikisha mianya yote ya upotevu wa fedha inadhibitiwa na kuzibwa ili kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali na hivyo kukuza kasi na ubora wa utoaji wa huduma kwa wananchi.
‘‘NBAA inatakiwa kuhakikisha kuwa wahasibu, wakaguzi hesabu na watu wote wanaofanya kazi za uhasibu na ukaguzi hesabu, wanafuata kanuni na miongozo ya uadilifu iliyotolewa na NBAA na pale ambapo itabainika kuwa kuna wanachama wanaokwenda kinyume na kanuni na miongozo hiyo basi hatua kali za kinidhamu zinachukuliwa ili kuwa fundisho kwa wahasibu na wakaguzi wote,’’alisema Bi. Omolo.
Bi. Omolo aliipongeza NBAA kwa ubunifu wa Namba ya Uhakiki Hesabu (NBAA Verification number - NBAAVN) ambayo itasaidia kuweka kumbukumbu za hesabu za fedha vizuri na hivyo kudhibiti mapato ya Serikali na mikopo chechefu kwenye taasisi za fedha.
Aidha, Bi Omolo alisema kuwa kutokana na ugunduzi wa rasilimali za madini, mafuta, na gesi nchini, NBAA inatakiwa kujipanga kuhakikisha nchi inapata wataalamu wa kutosha na wenye ujuzi na weledi unaohitajika katika nyanja ya uhasibu na ukaguzi wa hesabu za masuala ya madini, mafuta na gesi ili kuleta maendeleo yanayokusudiwa.
‘’Naipongeza NBAA kwa kutambua kuwa ongezeko la wahasibu litakuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha uchumi wa viwanda unaopiganiwa na Serikali ya Awamu ya Sita, kwani ujenzi na uendeshaji wake unahitaji usimamizi bora wa fedha,’’alisema Bi Omolo.
Aidha, alisisitiza NBAA kuboresha utendaji wa kazi na utoaji huduma kwa wateja wake ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Sita na kukabiliana na ushindani wa utandawazi.
Pia Bi. Omolo alisisitiza umuhimu kwa NBAA kuongeza wigo wa ufaulu katika mitihani yake na kubuni mbinu mbalimbali za kufanikisha hilo pamoja na kuhakikisha vyuo vinavyoandaa wataalamu vina walimu bora, weledi wa kutosha, vifaa bora vya kufundishia, na mazingira mazuri ya kusomea.
Aliongeza kuwa mbali na kuongeza idadi, mkazo mkubwa lazima uwekwe kwenye kuzalisha wataalamu wenye weledi wa hali ya juu na kuendelea kuzingatia suala la ubora wa wahitimu.
Bi. Omolo aliipongeza Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) kwa mchango wake mkubwa katika uandaaji wa bajeti ya Serikali kwa miaka mingi, huku akitaka bodi hiyo kuongeza juhudi katika kuongeza idadi na ubora wa wataalamu wa uhasibu nchini.
Awali akizungumza katika mahafali hayo Mwenyekiti wa Bodi ya NBAA CPA, Prof Silvia Shayo Temu, alisema kuwa NBAA imeanzisha Mfumo wa Namba Maalumu ya Uhakiki wa Taarifa za Hesabu Zilizokaguliwa NBAA (Verification Number - NBAAVN) uliozinduliwa rasmi Julai 1, 2025 kwa ajili ya ukusanyaji na uthibitishaji wa taarifa za hesabu zilizokaguliwa na kuwasilishwa moja kwa moja kwa NBAA.
‘‘Mfumo huu utaongeza uwazi, ufanisi na uhalali wa taarifa za kifedha kwa kuondoa changamoto zilizokuwepo kwenye mfumo wa zamani wa kutumia karatasi, ambao ulikuwa na mianya ya upotoshaji wa taarifa’’, alifafanua Prof. CPA Temu.
Alitoa wito kwa wadau nchini wakiwemo wahasibu, wakaguzi, mashirika ya umma na binafsi kuanza kutumia mfumo huo, na kuwasiliana na NBAA kwa msaada au maelezo ya ziada kwani mfumo huo utabadilisha kwa kiasi kikubwa namna taarifa za kifedha zinavyokusanywa, kuthibitishwa na kutumika kwa kuzingatia uwazi na uwajibikaji.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA CPA Pius Maneno, aliishukuru Wizara ya Fedha kwa ushirikiano mkubwa inaotoa kwa NBAA katika kufanikisha shughuli za kukuza na kuimarisha fani ya uhasibu na ukaguzi wa hesabu hapa nchini.
Alisema katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 1,233 walitunukiwa vyeti katika ngazi mbalimbali ikiwemo Shahada ya Juu ya Uhasibu, ngazi ya cheti, Stashahada ya Viwango vya Kimataifa vya Kihasibu, Stashahada ya Taaluma katika Ukaguzi wa Ndani pamoja na Astashahada ya Viwango vya Kimataifa vya Kihasibu, baada ya kufaulu mitihani yao iliyofanyika miezi ya Novemba, 2024, Februari, 2025, Mei, 2025 na Agosti, 2025.
No comments:
Post a Comment