
Na John Bera, Mwanza
Wanamichezo wapatao 436 wanaoshiriki Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) kwa Mwaka 2025, wametembelea Hifadhi ya Taifa ya Saanane iliyoko Mkoani Mwanza kwa ajili ya kujionea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyo hifadhini hapo.
Akizungumza mara baada ya kuwapokea wanamichezo hao, Afisa utalii wa Hifadhi ya Taifa ya Saanane, Bi. Cecillia Nkwabi, amesema ujio wa wanamichezo hao ni fursa ya kipekee kwa hifadhi hiyo kupokea watalii wa ndani.
Ameongeza kuwa ziara hiyo ni sehemu ya mkakati wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) wa kuongeza idadi ya Watanzania wanaotembelea hifadhi za taifa, sambamba na kuwawezesha Watanzania wengi kufurahia, kujifunza, na kutambua umuhimu wa rasilimali walizonazo hapa nchini.
"Lengo letu ni kuwawezesha Watanzania wengi kuzitambua na kuzithamini hifadhi zetu, kama sehemu ya burudani, elimu, kujenga uhusiano pamoja na kuongeza na kuimarisha pato la taifa kupitia utalii wa ndani," amesema Nkwabi
Sambamba na hayo, Bi. Nkwabi ameongeza kuwa wanamichezo hao wamepata fursa ya kufanya mazoezi wakiwa ndani ya hifadhi, huku wakifurahia mandhari ya asili ya kisiwa hicho, ikiwemo kuona wanyama kama simba, pofu na ndege wa aina mbalimbali wakiwemo tausi pamoja na kupanda boti kwa mara ya kwanza kwa baadhi yao.
"Wamefanya mazoezi kwa kutumia mandhari ya asili ya hifadhi. Wengine wamepanda boti kwa mara ya kwanza, wengine wamewaona tausi kwa mara ya kwanza. Haya yote ni uzoefu wa kipekee unaojenga kumbukumbu nzuri kwao," amesema.
Aidha, ametoa wito kwa washiriki wengine wa SHIMIWI ambao hawakupata nafasi ya kutembelea hifadhi hiyo, kuhakikisha wanaitembelea kabla mashindano hayajatamatika.
Kwa upande wao, baadhi ya wanamichezo waliotembelea hifadhi hiyo wameeleza kufurahishwa na kile walichojionea. Bw. Joachim Bugilo kutoka Taasisi ya Mifugo (LITA) amesema ameshuhudia maajabu ya uumbaji wa Mungu na namna ambavyo Serikali imewekeza katika kuhifadhi rasilimali hizi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Naye Kamimu Mratibu wa 'Maliasili Sport Club', Bw. George Rwezaura ameeleza kufurahishwa na vivutio vilivyopo katika hifadhi hiyo, vikiwemo maeneo ya kupumzikia kama Camp Sites, Jump Stone na Picnic Sites, ambayo ni mazuri kwa watu binafsi au familia kufanyia matukio mbalimbali yakiwemo sherehe za ubatizo, kipaimara, kuzaliwa, fungate au mapumziko ya mwisho wa mwaka.






No comments:
Post a Comment