WATAALAMU WA BAJETI WATAKIWA KUZINGATIA VIPAUMBELE VYA WANANCHI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, September 3, 2025

WATAALAMU WA BAJETI WATAKIWA KUZINGATIA VIPAUMBELE VYA WANANCHI



Na Angela Msimbira, OR-TAMISEMI


Maafisa bajeti wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa wametakiwa kuhakikisha mchakato wa uandaaji wa Mipango na Bajeti unazingatia vipaumbele vya wananchi pamoja na Sera za kitaifa ili kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Akitoa mada katika mafunzo ya uandaaji wa mipango na bajeti kwa maafisa bajeti, Mchumi Mwandamizi, Alfao Sanga, amesema bajeti ni nyenzo muhimu ya kusimamia matumizi ya rasilimali za Serikali na kufanikisha utekelezaji wa malengo ya maendeleo kwa wananchi.

Sanga amebainisha kuwa maandalizi ya bajeti yanapaswa kufuata hatua zilizowekwa kisheria kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, kata, halmashauri hadi bungeni kwa ajili ya kupitishwa rasmi.

“Wananchi wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika mchakato wa kupanga bajeti ili kuhakikisha mahitaji yao ya msingi kama afya, elimu, maji na miundombinu yanapatiwa kipaumbele,” amesisitiza

Ameongeza kuwa uandaaji wa bajeti unapaswa kuzingatia takwimu sahihi, usawa wa kijinsia pamoja na makundi maalum yakiwemo wanawake, vijana, watoto na watu wenye ulemavu ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inawanufaisha watanzania wote.

Kwa mujibu wa Sanga, bajeti inayotayarishwa kwa uwazi na ushirikishwaji huchangia kuimarisha uwajibikaji, kupunguza mianya ya matumizi mabaya ya madaraka na kuchochea maendeleo endelevu ya Taifa.

Jumla ya washiriki 415 walihudhuria mafunzo hayo yanayolenga kuwajengea uwezo maafisa bajeti wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini ili waweze kuandaa bajeti bora na shirikishi.




No comments:

Post a Comment