Na WMJJWM- Dodoma
Wizara zimetakiwa kujumuisha masuala ya kijinsia katika bajeti zao kwani ni jukumu la sekta zote ili kukuza usawa wa kijinsia nchini.
Hayo yamesemwa leo Septemba 3, 2025 Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia, Badru Abdunuru ambaye amemuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, wakati ufungaji wa mafunzo ya Ujumuishaji wa bajeti kwa maafisa wa Serikali kutoka Wizara mbalimbali.
Ameeleza kwamba ni muhimu kufanya kazi kwa kushirikiana kwani masuala ya kijinsia ni mtambuka na kila mmoja ana nafasi na mchango mkubwa sana katika kuimarisha hali ya usawa wa kijinsia nchini.
“Kupitia programu hii tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutekeleza masuala ya kijinsia katika Sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, maendeleo ya jamii pamoja na eneo la usimamizi wa mashauri ya ukatili wa kijinsia” amesema Badru
Ameongeza kwamba Wizara imeandaa mazingira wezeshi ya utekelezaji wa Ajenda hiyo ikiwemo kuratibu Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2023), Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA II 2024/25 – 2028/29), Jukwaa la Kizazi chenye Usawa, Ajenda ya Kitaifa ya kuwekeza katika Afya na Maendeleo ya Vijana Balehe, Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutekeleza Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama (2025 -2029) Kampeni ya Inspire to Lead na mambo mengine mengi.
Aidha amesema kuwa msisitizo wa kuzingatia masuala ya kijinsia katika Bajeti umezingatiwa pia kwenye Dira ya Taifa ya 2050, ambapo Nguzo ya Pili, shabaha ya 12 inasema “Tanzania kuwa kinara barani Afrika na miongoni mwa nchi kumi bora duniani katika kupunguza pengo la kijinsia kwa angalau asilimia 85” na ndiyo shabaha na dhamira ya Serikali katika kuimarisha usawa wa kijinsia na kuhakikisha kuwa kila mtanzania ananufaika na fursa zilizopo, anashiriki na anakuwa huru dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Naye Mwalilishi kutoka Umoja wa Ulaya (EU) Alexandra Pissat amesema ili kuleta usawa wa kijinsia ni muhimu kuzingatia bajeti katika masuala ya jinsia, kufanya tathmini na ufuatiliaji ili kuendelea kuondoka changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kurudisha nyumba mipango ya kuleta usawa wa kijinsia nchini.
"Mabadiliko chanya na maendeleo kwa jamii yanapatikana tu ikiwa usawa wa kijinsia unazingatiwa katika mipango ya Serikali katika utekelelezaji wa ajenda mbalimbali za kuwawezesha wanawake katika masuala ya jinsia." amesisitiza Alexandra
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Wizara ya Maji, Susan Magoti amesema mafunzo hayo yamekuwa msaada mkubwa kwani yanaelekeza kutoa kipaumbele katika kutenga bajeti kwa kuhusisha masuala ya usawa wa kijinsia jambo ambalo litachangia maendeleo na ushiriki wa wanawake katika uwezeshaji na uongozi.
Mafunzo hayo yalishirikisha washiriki zaidi ya 200 kutoka Wizara na Wakala za Serikali yakiandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU), yakilenga kutoa elimu ya ujumuishaji wa masuala ya jinsia katika bajeti ili kuleta usawa wa kijinsia, kuongeza uelewa na kuwapa washiriki zana, maarifa na ujuzi unaohitajika ili kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake katika mipango na bajeti za Wizara za kisekta, kwa kuzingatia Sera ya Jinsia 2023 na Dira ya 2050.
No comments:
Post a Comment