Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Kagera Faris Burhan ameahidi kuwa Vijana wa Tanzania watamlinda na kumsemea kwa wivu mkubwa Mgombea wa nafasi ya Urais ka tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa Vijana hawataingia kwenye mtego wa kushawishiwa kujiingiza katika matendo ya uvurugaji wa amani.
Burhan amebainisha hayo leo Alhamisi Oktoba 16, 2025 wakati wa Mkutano wa Kampeni za Mgombea Urais huyo kwenye Viwanja vya Kaitaba, Bukoba Mjini Mkoani Kagera, akiahidi pia Umoja huo kuendelea kuzitafuta na kuzilinda kura za Dkt. Samia kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Mwenyekiti huyo wa UVCCM Kagera amebainisha kuwa sababu ya kufanya hivyo ni kutokana na mafanikio makubwa na upendeleo aliouonesha Dkt. Samia kwa Vijana wa Kitanzania, hasa katika utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/25 akisema Ilani hiyo imetoa jawabu na kuwafuta machozi Vijana wa Tanzania dhidi ya changamoto ya ajira na ukuaji wa uchumi.
Aidha ameeleza pia kuhusu uwezeshaji mkubwa wa Vijana kiuchumi, akitolea mfano Mkoa wa Kagera na kusema kuwa takribani Shilingi Bilioni 15 za Mikopo zimetolewa kwa Vijana, wanawake na wenye ulemavu kutoka Shilingi Bilioni 3.2 zilizokuwa zinatolewa hapo awali kabla ya ujio wa serikali ya awamu ya sita.
Burhan amemtaja Dkt. Samia pia kama Mwalimu wa siasa za kikomavu, akisema kampeni zake zimekuwa somo la ustaarabu katika siasa za Tanzania suala ambalo limevutia Vijana wengi kufanya maamuzi ya kumpa kura za ushindi hapo Oktoba 29, 2025 siku ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment