
Na Mwandishi Wetu, Dar Es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, amesema kuwa mafunzo ya wanawake katika uongozi yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi yanalenga kuwajengea uwezo kundi hilo ili kuwa viongozi wazuri na wenye kuleta mabadiliko na maendeleo katika maeneo waliyopo.
Dkt. Jingu ameyasema hayo leo tarehe 07 Oktoba, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kongamano la Tano la Wanawake katika Uongozi lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute) chini ya dhima ya ‘Mchango wa wanawake katika uongozi barani Afrika’.
Dkt. Jingu amesema ni ukweli uliowazi kuwa viongozi wanatengenezwa hivyo Taasisi ya Uongozi inaendeleza adhima hiyo kwa kutoa mafunzo ili kupata wanawake wakaoshika nafasi za juu za uongozi si kwa sababu za kijinsia bali kutokana na uwezo na sifa walizonazo.
“Msingi wa hayo yote haya ni kwamba viongozi wazuri wanatengenezwa, pamoja na kwamba baadhi wanaweza kuwa wamezaliwa na vipaji mbalimbali na uwezo wa kiuongozi, wakitengenezwa na kujengewa sifa zinazoitajika wanaweza kutoa mchango mzuri zaidi wa maendeleo katika maeneo au sekta walizopo,” amesema Dkt. Jingu
Aidha amesema kupitia mafunzo hayo wanatengeneza waleta mabadiliko katika jamii na kwamba wanawake kwa wanaume wakishirikiana katika shughuli za maendeleo basi mafanikio yatakuwa makubwa na changamoto zilizopo katika jamii zitapungua au kuisha kabisa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo amesema programu mpya ya Wanawake katika Uongozi imelenga kuwajengea uwezo wanawake ili wanapochukua nafasi za kiuongozi waweze kuzitumia vyema na hatimaye kuongeza uwakilishi wa wanawake katika nafasi za juu za kisiasa, kiuchumi na kibiashara.
“Mwitikio wa wanawake kushiriki mafunzo haya umekuwa mkubwa, miaka ya nyuma tunapotangaza kuanza kwa kodi waliokuwa wanaomba walikuwa kati ya 500 hadi 600, mwaka huu walioomba viongozi kutoka barani Afrika ni 2009 ila waliopata ni 100, kati ya watu hao walioomba wanatoka Botswana, Namibia, Cameroon, Kenya, Uganda, Marekani, Uingereza na Sweden,” amesema Singo
Washiriki wa kongamano hilo wametoka katika nchi mbalimbali ikiwemo Kenya, Afrika Kusini, Namibia, Cameroon, Rwanda, Gambia, Zambia, Nigeria, Liberia, na mwenyeji Tanzania.


No comments:
Post a Comment