
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuendelea kuziunganisha Wilaya za Mkoa wa Simiyu kwa barabara za lami na Makao makuu ya Mkoa pamoja na Barabara kuu za Kata zinazoelekea kwenye makao makuu ya Wilaya za Mkoa huo wa Kanda ya Ziwa.
Dkt. Samia pia amewataka Vijana wa Maswa Mkoani Simiyu kujiandaa kutumia vyema fursa zinazotokana na ujio wa reli ya kisasa ya SGR Wilayani humo pamoja na ujenzi wa Kituo cha kushusha na kupakia abiria na mizigo katika Wilaya hiyo, akisema miundombinu hiyo itakuja na fursa za ajira na uchumi kwa wananchi wa Maswa.
Mgombea Urais huyo amebainisha hayo leo Jumamosi Oktoba 11, 2025 wakati akiendelea na kampeni zake kwenye Wilaya ya Maswa, akiahidi pia kuendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuondoa changamoto ya wanyamapori vamizi, ambao wamekuwa wakitoka katika maeneo yao ya hifadhi na kuvamia wananchi pamoja na mashamba yao ya kilimo.
Dkt. Samia ameahidi kuendelea kujenga vituo vya askari wanyamapori kwaajili ya kudhibiti wanyama hao pamoja na ununuzi wa vifaa mbalimbali vya ufuatiliaji ikiwemo ununuzi wa ndege nyuki kwaajili ya utambuzi na ufuatiliaji wa wanyama wanaotoka kwenye maeneo yao.





No comments:
Post a Comment