
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewahakikishia wananchi wa Karagwe Mkoani Kagera kuwa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali inaendelea kwa kasi ili kuboresha maisha yao.
Akizungumza wakati wa Mkutano wake wa kampeni leo Oktoba 15, 2025 kwenye Viwanja vya Bashungwa Wilayani Karagwe, Dkt. Samia amesema Serikali yake pia imekamilisha na kuendelea na miradi muhimu ya afya, barabara, elimu, biashara, michezo na nishati, ambayo inalenga kuleta maendeleo ya kweli katika kila kona ya wilaya.
Hadi sasa, vituo viwili vya afya vya Nyabiyonza na Nyakakika na zahanati 11 katika maeneo mbalimbali vimekamilika huku pia barabara kadhaa zikirekebishwa au kujengwa upya, ikiwa ni pamoja na barabara za Kajunguti- Rubale- Misha, Bujara- Kahanga, Nyakasimbi- Kigando- Nyaishozi, pamoja na ujenzi wa Bugene- Kasulo wenye urefu wa kilomita 124 na kipande cha Bugene- Burigi cha kilomita 60 kwa kiwango cha lami.
Sekta ya biashara pia inaendelea kuimarika kupitia ujenzi wa ukumbi wa mikutano Kayanga, vyumba vya biashara 84 katika Bugene na Nyaishozi, pamoja na upimaji na uuzaji wa viwanja Kihanga. Katika elimu, Serikali inatekeleza ujenzi wa vyumba vya madarasa 210, matundu ya vyoo 936, mabweni 10, na nyumba 20 za walimu, suala linalosaidia katika kuhakikisha shule za msingi na sekondari zinatoa elimu bora na mazingira salama kwa wanafunzi.
Pia, ujenzi wa uwanja wa michezo Kayanga unaendelea, huku mradi wa nishati ya umeme ukiwajumuisha wananchi kupitia kituo cha kupooza umeme Benaco wilayani Ngara na laini ya kusafirisha umeme kwa msongo wa 220 kilovolti hadi Kyaka.
Dkt. Samia amesisitiza kuwa miradi hii inalenga kuboresha huduma za jamii, kuongeza fursa za kiuchumi, na kuhakikisha kila mwananchi anafaidika na maendeleo endelevu. “Tunaendelea kuhakikisha kila kona ya Karagwe inafaidika na miradi ya maendeleo, huku tukiboresha maisha ya wananchi kwa huduma bora,” amesema Dkt. Samia.





No comments:
Post a Comment