
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Ijumaa Oktoba 03, 2025 anaingia siku yake ya tatu ya Kampeni Mkoani Arusha, akitarajiwa kufanya Mkutano wa hadhara wa Kampeni Wilayani Karatu na baadaye akitarajiwa kuanza ziara yake ya kikazi Wilayani Hanang Mkoani Manyara.
Akiwa Jijini Arusha kwenye Viwanja vya Sheikh Amri Abeid, Dkt. Samia ameeleza kuhusu dhamira yake ya kuendelea kukuza Utalii wa Mkoa wa Arusha kwa kujenga miundombinu na kuboresha uwanja wa ndege Arusha na Lake Manyara Karatu, kuongeza idadi ya ndege, kujenga Kituo cha Taarifa za Utalii na Kituo cha Ikolojia Ngororongo pamoja na ukuzaji wa Utalii wa michezo Mkoani Arusha, ujenzi wa Mji wa Bondeni City pamoja na masoko ya wafanyabiashara wadogo Bondeni city, Kilombero na Morombo.
Dkt. Samia kadhalika amesisitiza dhamira ya Chama Cha Mapinduzi ya ujenzi wa Ukumbi mkubwa wa kimataifa wa Mikutano Mkoani Arusha utakaokuwa na uwezo wa kuhudumia watu zaidi ya 6, 000 kwa wakati mmoja pamoja na kuendelea kuvutia na kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya Tanzania kuja Mkoani Arusha na kuwekeza kwenye ujenzi wa Hoteli, ili kutoa hakikisho la malazi kwa wageni na watalii mbalimbali.
Ilani ya 2025/30 anayoinadi Dkt. Samia imeahidi ujenzi wa majengo ya wagonjwa mahututi, dawa, Mama na mtoto na chumba cha kuhifadhia maiti kwenye Hospitali ya Wilaya ya Monduli, ujenzi na ukamilishaji wa vituo vinne vya afya na Zahanati 10, ujenzi wa daraja na barabara ya Makuyuni- Lemooti, Ujenzi wa shule mpya 3 za sekondari, mabweni 90, ujenzi wa vyumba 100 vya madarasa, Ujenzi wa mradi wa majisafi wa Monduli- Enguiki, Ujenzi wa Bwawa la Nanja, Mradi wa maji Sanganano, Tukusi pamoja na mradi wa uendeleza wa kupunguza hewa ya kaboni katika Vijiji 40 vya Halmashauri ya Wilaya ya Monduli.
Kwa Karatu, CCM imeahidi ujenzi wa Zahanati 5 na Vituo vya afya 2, Ujenzi wa madaraja 3 katika barabara ya Endabash- Manyara, ujenzi wa madarasa 263 katika shule za Msingi na sekondari, Ujenzi wa maabara 34 kwenye shule za sekondari, ununuzi wa zana za kilimo (powertiller 10), ujenzi wa miundimbinu 3 ya umwagiliaji, ujenzi wa miradi ya maji Gyekrum Lambo, Oldean na Kiwanja, Qurus, ukarabati wa majosho 13, ujenzi wa machinjio 1 ya Kuku, Ujenzi wa madaraja/ Vivuko 9, ununuzi wa mashine 4 za boti za uvuvi na Maboresho ya mialo 1 ya samaki kwenye Ziwa Eyasi.

No comments:
Post a Comment