DKT. SAMIA KUTIMUA VUMBI MKURANGA, KIBITI NA RUFIJI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, October 20, 2025

DKT. SAMIA KUTIMUA VUMBI MKURANGA, KIBITI NA RUFIJI


Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumatatu Oktoba 20, 2025 anatarajiwa kuanza Kampeni zake Mkoani Pwani, akipangiwa kuwa na Mikutano Mitatu kwenye Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji, ili kuinadi Ilani ya Chama chake na kuomba kura kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Katika Mkoa wa Pwani serikali ya Dkt. Samia ndani ya Miaka minne imefanikiwa kukamilisha mradi wa ujenzi wa bwawa la Kufua umeme la Julius Nyerere ambalo linachangia Megawati 2,115 kwenye Gridi ya Taifa, kukamilisha ujenzi wa daraja jipya la Wami lenye urefu wa Mita 513.5 na upana wa Mita 11.85 pamoja na kukamilisha miradi mitatu ya soko la kisasa la samaki Bagamoyo, Soko la kisasa (Shopping mall) ya Kibaha pamoja na ujenzi wa Kituo cha Kisasa cha Mabasi Chalinze Mkoani Pwani.

Serikali ya awamu ya sita pia imefanikiwa kuongeza Vituo vya kutolea huduma za afya Mkoani Pwani ikiwemo Hospitali za Wilaya kutoka 10 hadi 14, Vituo vya afya kutoka Vituo 43 hadi 53, Zahanati 413 kutoka 319 za awali pamoja na maboresho makubwa ya utoaji wa huduma kwenye Hospitali ya rufaa Mkoa wa Pwani, Tumbi.

"Kwa Tumbi tunamshukuru Mhe. Samia kwasababu amefanya ukarabati na kuweka vifaa vya kisasa katika Jengo la dharura, ujenzi wa Vyumba vya wagonjwa mahututi, Vyumba vya kitengo cha kuchuja damu na jengo la wagonjwa wa nje pamoja na kuongeza upatikanaji wa dawa, vifaatiba, vifaa na vitendanishi katika Vituo vya kutolea huduma za afya kutoka asilimia 88.92 hadi asilimia 92.21" amesema John Akalisa, Mdau wa maendeleo Kibaha.

Kuelekea mwaka 2030 pamoja na mambo mengine Ilani anayoinadi Dkt. Samia imeahidi ukamilishaji wa Zahanati 27 na Ujenzi wa Zahanati mpya 50 na Vituo 12 vya afya kwenye Wilaya ya Mkuranga, Ujenzi wa shule mpya tatu za Msingi za Mwandege, Vikindu na Vianzi na shule 4 za Sekondari huko Kizapala, Mponga, Dondwe na Mwandege pamoja na ujenzi na upanuzi wa miradi mbalimbali ya maji na uchimbaji wa visima 30 kwenye Vijiji vya Mkuranga.

Kwa Rufiji CCM inaahidi ujenzi wa Hospitali kubwa ya Kanda Kata ya Mbwara Nyamwage, ujenzi wa barabara za lami za Kilomita 10 Mji wa Utete na Kilomita 20 Mji wa Ikwiriri, Ujenzi wa soko la Kisasa Tarafa ya Ikwiriri, Ujenzi wa Kituo cha mabasi Ikwiriri, ujenzi wa masoko madogo Shela, Mwaseni, Ngorongo na Mbwara pamoja na ujenzi wa Vituo 6 vya mafunzo ya walimu huko Chumbi, Mibuyusaba, Mgomba, Nyaminywiri, Mapinduzi na Nyamwange.

Aidha kwa Kibiti Ilani ya 2025/30 imeahidi ununuzi wa mashine 5 za Xray kwenye Vituo vya afya Kibiti, Mjawa, Kivinja, Mbwera na Nyamatanga, Ujenzi wa soko la Kisasa Kibiti, Ujenzi wa karakana na maabara za Kilimo kwenye shule za Sekondari Mtawanya na Nyambili zenye mchepuo wa amali, Ujenzi wa ghala la kisasa Kibiti, Ujenzi wa jengo la maonesho ya Nanenane, ujenzi wa malambo 6, Machinjio ya kisasa Kibiti, ujenzi wa fukwe Vijiji vya Jaja, Simbaulanga na Pombwe pamoja na ukamilishaji wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kitongoji cha Lumyozi.

No comments:

Post a Comment