
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumanne Oktoba 07, 2025 anatarajiwa kuendelea na Kampeni za Uchaguzi Mkuu Kanda ya Ziwa akianza na Mkoa wa Mwanza kwenye Wilaya za Misungwi, Sengerema na Wilaya ya Nyamagana.
Dkt. Samia Suluhu Hassan anaingia kwenye Kanda ya Ziwa akitokea Kanda ya Kaskazini, Mwanza ikiwa Mkoa wake wa 21 wa Kampeni ambapo akiwa Manyara mwishoni mwa Wiki iliyopita, Dkt. Samia ameahidi mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukuza kilimo cha Ngano Wilayani Hanang, kuendeleza sekta ya madini pamoja na kuimarisha na kutangaza utalii wa Mkoa huo ili kuendelea kuzalisha fursa za ajira na kukuza kipato cha wananchi wa Mkoa huo.
Katika Ilani anayoinadi Dkt. Samia Kwa Wilaya ya Nyamagana, wameahidi ujenzi wa Jengo la matibabu ya Ubongo na mishipa ya fahamu na jenzi wa Jengo la huduma za utumbo na ini Hospitali ya Bugando, Ujenzi wa jengo la matibabu na upandikizi figo pamoja na kununua vifaa tiba vya vipimo na maabara kwa mashine ya MRI na Fluoroscopy kwenye Hospitali hiyo, ujenzi wa jengo la dharura na jengo la wagonjwa wa nje katika Hospitali ya Mkoa Seketoure pamoja na ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka awamu ya IV na VI katika maeneo ya Ziroziro- Airport, Ziroziro- Nyashishi na Ziroziro- Kisesa.
Kwa Wilaya ya Misungwi CCM imeahidi kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, Kukamilisha ujenzi wa Zahanati 30 kwenye Vijiji mbalimbali, Kukamilisha ujenzi wa Vituo vya afya Nhundulu na Usagara, Ujenzi wa soko na Kituo cha mabasi madogo Nyashishi, Ujenzi wa Kituo kikuu cha mabasi Misungwi, ujenzi eneo la maegesho ya magari ya Mizigo Usagara pamoja na ujenzi wa shule mpya nne za Sekondari Kata ya Igokelo, Usagara, Misungwi na Mbarika pamoja na ujenzi wa shule mpya za msingi kwenye Kata za Misungwi, Usagara na Igokelo.
Katika Wilaya ya Sengerema, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM (2025/30), imemuelekeza Dkt. Samia ikiwa atapata ridhaa ya kuunda serikali kuongeza taa 237 za barabarani, upanuzi wa miradi ya maji Sengerema, Nyitundu, Kazunzu Lubanda, Irunda, Ngoma, Tunyenye na Kishinda, utafiti na uchimbaji wa visima 38, Utekelezaji wa mradi wa mtandao wa majitaka Mjini Sengerema, ujenzi wa majosho na malambo 5 ya mifugo, uanzishaji wa mashamba darasa 10 ya malisho pamoja na ujenzi wa vibanio 15 vya matibabu na chanjo kwa mifugo kwenye Vijiji zaidi ya 13 vya Wilaya ya Sengerema.

No comments:
Post a Comment