Leo Alhamisi Oktoba 23, 2025, Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuendelea na Kampeni zake za Uchaguzi Mkuu Jijini Dar Es Salaam kwa kuwa na Mkutano wa hadhara wa Kampeni eneo la Buza Tanesco, Wilayani Temeke.
Dkt. Samia anaingia Wilaya ya Temeke ikiwa ni siku yake ya mwisho ya Kampeni Mkoani humo akitokea kwenye Wilaya za Kinondoni na Ilala, ahadi zake kubwa zikiwa ni kuendelea kuijenga na kuiimarisha miundombinu ya Maji safi na Majitaka, Miundombinu ya usafiri na usafirishaji pamoja na kuendelea kusogeza huduma za Kijamii karibu zaidi na wananchi wa Mkoa huo.
Miongoni mwa Sekta kubwa ambayo ameahidi kuifanyia kazi ni sekta ha Maji ambapo katika Kipindi cha miaka minne iliyopita Jiji hilo limeshuhudia uongezekaji wa Upatikanaji wa huduma hiyo kutoka asilimia 80 hadi 93 ikitokana na kukamilika kwa miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa maji Kimbiji, Pugu Gongolamboto, Mshikamano na upanuzi wa mradi wa maji wa Dar Es salaam Kusini na kuongezeka kwa mtandao wa usafirishaji na usambazaji wa majisafi kutoka Kilomita 3,015 hadi 6,608.
Aidha Mafanikio mengine yaliyopatikana ndani ya Miaka minne ya serikali ya awamu ya sita ni pamoja na kupungua kwa upotevu wa maji yasiyolipiwa kutoka asilimia 48
3 hadi asilimia 32, kuongezeka kwa idadi ya maunganisho ya majisafi kutoka kwa Wateja 265,712 hadi wateja 489,581, kuongezeka kwa uwezo wa kuhifadhi maji kutoka Mita za ujazo 88, 375 hadi Mita za ujazo 207, 965 na kuongezeka kwa muda wa upatikanaji wa maji Dar Es Salaam kutoka wastani wa saa 15 kwa siku hadi kufikia saa 21 za upatikanaji wa maji kwa siku.
Kuongezeka kwa saa hizo za upatikanaji wa maji kumetokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali ikiwemo ujenzi wa tenki lenye uwezo wa kuhifadhi maji zaidi ya Lita Milioni 15 huko Kigamboni, mradi uliogharimu zaidi ya Bilioni 25, suala ambalo mbali ya kuhakikishia upatikanaji wa maji wananchi wa Kata 7 za Kigamboni, Mradi huo pia umepunguza gharama za maji kwa wananchi waliokuwa wakilazimika kununua maji kwa gharama kubwa kutoka kwa watu binafsi waliokuwa na visima vya maji.
Salma Ramadhani na Mzee Ali Seif wameishukuru serikali kwa utekelezaji wa mradi huo, wakisema sasa familia zao pia hawalazimiki kuamka alfajiri sana ama usiku wa manane kwenda kufuata huduma ya maji, Wito ukitolewa kwa wananchi kuendelea kuunga huduma hiyo kwenye makazi yao ili kuzidi kutoa unafuu katika upatikanaji wa maji karibu zaidi na familia.
No comments:
Post a Comment