
Na Mwandishi Wetu – Dodoma
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) leo, Oktoba 6, 2025, imezindua Wiki ya Huduma kwa Mteja kwa kuanza na mafunzo maalum kuhusu Afya ya Akili na Huduma kwa Mteja kwa watumishi wake.
Katika mafunzo hayo, DUWASA imeshirikiana na wataalamu wa afya ya akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe pamoja na Mtaalamu wa Saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Chris Mauki.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph, amewataka watumishi wa Mamlaka hiyo kutoa huduma bora kwa wateja kwa kuzingatia heshima na weledi.
“Sisi tuko mjini, Serikali inatuangalia, wateja wetu wanatuangalia. Ni lazima kuhakikisha tunafikia ahadi ya asilimia 95 ya upatikanaji wa huduma za majisafi. Tumefanya kazi kubwa, bado kuna changamoto, lakini tuna fursa ya kuboresha zaidi huduma zetu,” alisema Mhandisi Aron.
Aidha, alisisitiza kuwa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja ni fursa muhimu kwa DUWASA kusikiliza maoni ya wateja, kujitathmini katika utendaji wake, na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho.
Mbali na mafunzo hayo, DUWASA pia imetoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa wagonjwa na wahitaji katika Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, ikiwa ni sehemu ya uwajibikaji kwa jamii.
Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja yalianza rasmi leo na yanatarajiwa kukamilika Oktoba 12, 2025, yakiwa na kaulimbiu isemayo:“Dhamira Inawezekana.”








No comments:
Post a Comment