Elimu ya Matumizi Sahihi ya Mbolea Yawapa Matumaini Wakulima Njombe - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, October 4, 2025

Elimu ya Matumizi Sahihi ya Mbolea Yawapa Matumaini Wakulima Njombe


Wakulima wa Kijiji cha Miva mkoani Njombe wamefurahishwa na elimu ya matumizi sahihi ya mbolea inayotolewa na Wizara ya kilimo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kama sehemu ya maandalizi kuelekea msimu wa kilimo wa mwaka 2025/2026.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Miva, Auleris Mlelwa, amebainisha hayo wakati wa mkutano uliowakutanisha wataalam kutoka Wizara ya Kilimo, TFRA, Ofisi ya Mkoa wa Njombe, Idara ya Kilimo na Mifugo Halmashauri ya Mji Njombe, wadau wa mbolea pamoja na wakulima mara baada ya kupatiwa mafunzo hayo.

“Hapa kinachofanyika si tu kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea, bali pia wataalam wanatoa maarifa mbadala yatakayosaidia wakulima kuepuka kuchanganya mbolea hovyo bila ushauri wa kitaalam,” amesema Mlelwa.

Akitoa elimu hiyo kwa wakulima, Joshua Ivan, Bwana Shamba kutoka kampuni ya OCP Tanzania, amewataka wakulima kuzingatia namba zinazoonekana kwenye mifuko ya mbolea huku akibainisha zimebeba maana kubwa sana

Akiongea kwa mfano, Joshua amesema virutubisho vilivyopo kwenye mbolea aina ya NPK 25:05:25, namba ya kwanza - 25 huashiria virutubisho kwa ajili ya ukuaji wa majani, 05 ni kwa ajili ya kuimarisha mizizi wakati 25 ya mwisho ni kwa ajili ya kuimarisha matunda na hivyo mkulima anapaswa kuzingatia anapoweka mbolea anakusudia kuimarisha eneo lipi la mmea.

Kwa upande wake, Afisa Masoko wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), Samwel Msongwe, amewahakikishia wakulima upatikanaji wa mbolea katika maeneo yao kwa msimu huu wa kilimo huku akisisitiza kuwa, kampuni hiyo imejipanga kusogeza pembejeo karibu zaidi na wakulima.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent, amesema kuwa lengo la kuwafikia wakulima wa viazi mkoani humo ni kujifunza namna wanavyojishughulisha na kilimo kutokana na Njombe kuwa kinara wa uzalishaji na matumizi ya mbolea nchini.

Ameeleza kuwa, matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka tani 365,000 mwaka 2022/2023 hadi kufikia tani 972,000 katika msimu wa kilimo 2024/2025, na yanatarajiwa kukua zaidi hadi kufikia tani milioni 1.1 katika msimu wa kilimo 2025/2026.

Laurent amebainisha kuwa, ongezeko hilo limechangiwa na ruzuku ya mbolea inayowezeshwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ametajwa kama mkulima namba moja na mwenye kujali wakulima kwa vitendo.






No comments:

Post a Comment