JAMII YASISITIZWA KUHESHIMU MILA NA DESTURI ZAO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, October 20, 2025

JAMII YASISITIZWA KUHESHIMU MILA NA DESTURI ZAO



Jamii za Kitanzania zimesisitzwa kuheshimu, kulinda na kurithisha mila na desturi zao pamoja na kuzingatia maadili ya Taifa yanayoambatana na upendo, amani, utulivu na mshikamano nchini.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Amos Makala Oktoba 20, 2025 wakati akifungua sherehe za kiutamaduni za rika la vijana wa jamii ya Maasai wa Mkoa huo na Manyara zilizofanyika katika Boma Maalumu eneo la Arumeru.

Katika sherehe hizo, Vijana wa Mkoa wa Arusha, Manyara na Mikoa mingine nchini hukusanyika katika eneo maalumu ikiambatana na vijana hao kupewa baraka na kufanyiwa tambiko maalumu ikiwa ni uzinduzi rasmi wa msimu wa tohara kwa vijana hao utakaodumu kwa miaka saba (2025-2032).

Mhe. Makala alisema, kuna umuhimu wa kuendeleza mila hizo ili utamaduni wa Mtanzania uendelee kuwa hai na kurithishwa kutoka vizazi hadi vizazi.

"Watanzania tunapaswa kulinda mila na desturi zetu, ndio maana Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwa na dhamira ya dhati katika kukuza na kuendeleza shughuli za Sekta ya Utamaduni na Sanaa kitaifa na kimataifa pamoja na kuhakikisha kuwa wananchi wanapata fursa ya kusherehekea na kurithisha mila na tamaduni zao" alisisitiza Mhe. Makala.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Utamaduni Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Mnata Resani alisema Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kwa kusheheni utajiri wa uanuwai wa urithi wa utamaduni usioshikika uliofumbatwa katika lugha za asili kama kibebeo cha urithi, mila na desturi, matambiko na sherehe za kijadi, Sanaa na muziki wa asili, ngoma, majigambo, nyimbo, soga, utani, kazi za mikono za kiutamaduni, maarifa na ujuzi wa asili ambao jamii inapaswa kuuenzi na kuendelea kurithisha kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.










No comments:

Post a Comment