
Kamishna wa Madini, Dkt. AbdulRahman Mwanga, ameongoza kikao muhimu cha kitaalamu kati ya Wizara ya Madini, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), na kampuni ya utafiti ya Sismo Elettrica kutoka Italia, kilichofanyika leo, Oktoba 10, 2025, katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Madini, Mtumba jijini Dodoma.
Katika kikao hicho, Dkt. Mwanga ameipongeza timu ya wataalamu kutoka kampuni ya Sismo Elettrica kwa kuonesha nia ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kufanikisha tafiti za kisasa za kijiosayansi, hatua ambayo ni muhimu katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Sekta ya Madini nchini.
“Dira yetu ni kwamba Madini ni Maisha na Utajiri. Tumepanga ifikapo mwaka 2030, angalau asilimia 50 ya eneo lote la Tanzania liwe limefanyiwa utafiti wa kina wa High Resolution Airborne Geological Survey ikilinganishwa na hali ya sasa ambapo ni asilimia 16 pekee ndio imefanyiwa tafiti hizo ,” amesema Dkt. Mwanga.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Sismo Elettrica, Francisco Cintoch, amesema kuwa kampuni hiyo ina uzoefu mkubwa katika shughuli za utafiti wa madini barani Afrika, ambapo tayari imefanya kazi nchini Ghana na Nigeria kwa mafanikio makubwa.
“Tuna teknolojia ya kisasa ya kuchunguza madini kwa kutumia mbinu za upimaji wa mbali (remote sensing), ramani za anga, na mbinu za kifizikia za ardhini. Tunaamini utaalamu wetu utaisaidia Tanzania kufikia malengo yake ya kimkakati katika sekta hii,” amesema Cintoch.
Cintoch amesema kuwa, kwa sasa Kampuni ya Sismo Elettrica imesaini Hati ya Makubaliano na Vyuo Vikuu mbalimbali ili kuongeza ufanisi, weledi na uwazi katika shughuli za utafiti ambapo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Siena, Italy na Chuo Kikuu cha Florence Italy.
Naye Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Siena cha nchini Italia, Prof. Ricardo Salvini, ambaye pia ni mshirika wa kampuni hiyo, amesema wataalamu wa Sismo Elettrica wana uwezo mkubwa wa kufanya tafiti za kijiolojia kwa kutumia njia za kisayansi na teknolojia ya hali ya juu.
“Tunatumia mbinu za juu (aerial surveys) kwa kutumia ndege na drone pamoja na vipimo vya kifizikia vya ardhini ili kubaini maeneo yenye utajiri wa madini kwa haraka na kwa usahihi mkubwa,” ameeleza Prof. Salvini.
Kikao hicho ni sehemu ya juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Madini kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na taasisi za kitaalamu katika kuhakikisha rasilimali za madini nchini zinaletwa kwenye mchango wa maendeleo ya taifa kwa njia endelevu.





No comments:
Post a Comment