
Mkuu wa Mkoa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, akizungumza na wananchi wa Maisaka kuhusu malipo ya fidia ya maeneo yao yaliyotwaliwa kwa matumizi ya huduma za kijamii.


Mhe. Queen Sendiga, Mkuu wa Mkoa Manyara, akitoa ufafanuzi kwa wananchi kuhusiana na utekelezaji wa malipo ya fidia kwa kaya za Maisaka.
Na Mwandishi Wetu.
BABATI, MANYARA – Kaya ishirini na nane (28) za maeneo ya Msasani Maisaka A na Maisaka Kati, Wilayani Babati mkoani Manyara hatimaye zimelipwa fidia ya jumla ya shilingi bilioni 2.9 baada ya maeneo yao kutwaliwa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya huduma za kijamii, ikiwemo uhifadhi wa vyanzo vya maji katika eneo hilo.
Malipo hayo yamethibitishwa kupitia kikao kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara Oktoba 23, 2025, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga aliongoza majadiliano kati ya wananchi na viongozi wa Serikali.
Wananchi walioshuhudia tukio hilo wameeleza kufarijika baada ya kusubiri kwa muda mrefu tangu mwaka 2008 bila kujua mustakabali wa maeneo yao. Wamesema malipo hayo ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutatua changamoto za wananchi kwa vitendo.




"Tumengoja zaidi ya miaka 15 bila majibu. Leo tunapokea haki yetu. Tunamshukuru Mhe. Queen Sendiga kwa kufuatilia suala hili kwa ukaribu hadi tumepata fidia yetu," alisema mmoja wa wanananchi waliolipwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga aliwashukuru wananchi hao kwa kuridhia kuachia maeneo hayo kwa manufaa ya jamii pana ya Wilaya ya Babati, kwani eneo hilo ni chanzo muhimu cha maji kinachohudumia wakazi wengi.
"Nawapongeza kwa moyo wa kizalendo na uelewa mlioonesha kwa kuweka mbele maslahi ya jamii nzima. Serikali imezingatia haki zenu, na leo tumeshuhudia kulipwa kwa fidia hii ili mradi wa kuhifadhi na kuboresha chanzo cha maji uendelee," alisema Mhe. Sendiga.
Aidha, Mhe. Sendiga alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha wananchi wanaoshiriki katika kutekeleza miradi ya maendeleo wanahakikishiwa haki zao, huku akitoa wito wa kuendelea kulinda na kuheshimu maeneo ya vyanzo vya maji ili kuimarisha upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.
Tukio la malipo hayo limepokelewa kwa matumaini mapya ya maendeleo na ushirikiano baina ya wananchi na Serikali, hususan katika kulinda rasilimali za asili zinazochangia ustawi wa maisha ya jamii.



No comments:
Post a Comment