KIWANDA CHA KUSAFISHA DHAHABU CHUNYA MBIONI, SERIKALI YATIMIZA AHADI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, October 9, 2025

KIWANDA CHA KUSAFISHA DHAHABU CHUNYA MBIONI, SERIKALI YATIMIZA AHADI



Na Mwandishi Wetu, Chunya


Chunya, Mkoa wa Pili wa Kimadini kwa uzalishaji wa dhahabu nchini baada ya Geita, imepiga hatua kubwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Kiwanda cha Kusafisha Dhahabu cha Giant Equipment and Machine’s Limited. Kiwanda hiki kina uwezo wa kusafisha kilo 20 za dhahabu kwa siku kwa usafi (purity) wa asilimia 99.9 na kiko mbioni kuanza uzalishaji rasmi, baada ya kukamilika kwa baadhi ya taratibu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) .

Akizungumza katika mahojiano maalum na timu ya Madini Diary kutoka Wizara ya Madini Oktoba 8, 2025, Meneja Uendeshaji wa Kampuni hiyo Hassan Pazi amesema tayari majaribio ya kusafisha dhahabu kiwandani hapo yamefanyika kwa awamu tatu tofauti na zote zimetoa matokeo ya kiwango cha kusafisha hadi asilimia 99.9, jambo linaloashiria kuwa dhahabu inayosafishwa na kiwanda hicho inakidhi vigezo vya kununuliwa na BoT kutumika kama amana ya Serikali na kusafirishwa nje.

‘’Awamu zote zilionesha purity ya asilimia 99.9 hii ni kiashiria tosha kwamba mashine zetu ziko vizuri na tumefikia lengo letu hivyo, wachimbaji wawe tayari muda si mrefu tutaanza rasmi kusafisha dhahabu hapa Chunya. Kwa sasa zipo taratibu tunazikamilisha na BoT,’’ amesema Pazi.

Ameongeza kwamba, hatua ya Chunya kuanza kusafisha dhahabu itasaidia kupunguza adha ya wachimbaji na wafanyabiashara kusafiri umbali mrefu hadi katika mikoa ya Dodoma, Geita na Mwanza kwa ajili ya kupata huduma hiyo.

Kutokana na hatua iliyofikiwa na kampuni hiyo, imeipongeza Serikali kwa kutoa eneo ambalo limewezesha kujengwa kwa kiwanda hicho ikiwemo kutembelewa mara kwa mara na wataalam kwa ajili ya ushauri na maelekezo yaliyowezsha kukamilisha taratibu zote.

Akizungumzia kuhusu ajira, Pazi amesema kiwanda hicho kitaendeshwa kwa asilimia 100 na watanzania na kwamba watalamu wa kitanzania walihusika katika hatua zote tangu ujenzi kikihusisha wahandisi, watoa huduma na wajenzi hadi kufikia hatua ya kuelekea kwenye uzalishaji.

Mbali na kusafisha dhahabu, kampuni hiyo inamiliki kiwanda cha kuchenjua dhahabu chenye mitambo ya uwezo wa kubeba kilo 650 za kaboni kila mmoja. Pia, kampuni hiyo inajihusisha na biashara ya kuuza kemikali za aina zote, vifaa kinga na kudhamini wachimbaji wadogo.

Kukamilika kwa kiwanda hicho kunaendelea kuonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya kuongeza thamani ya madini hapa nchini na kutekeleza mikakati ya sekta hiyo kwa vitendo. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alikielezea kiwanda hicho bungeni katika hotuba ya bajeti ya mwaka 2025/26 na sasa, ahadi hizo zimetia mwanzoni tu mwa robo ya pili ya mwaka.

Mbali na kuongeza ajira na kukuza uchumi wa Chunya, Serikali itanufaika kupitia kodi na tozo mbalimbali sambamba na Halmashauri ya Wilaya ambayo itanufaika moja kwa moja na mapato yatokanayo na shughuli za kiwanda.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mhe. Mbarak Alhaji Batenga akizungumza na Madini Diary Oktoba 9, 2025 amesema uwepo wa Kiwanda hicho kitasaidia kuongeza thamani ya dhahabu inayozalishwa Chunya na kuufanya Mkoa huo wa Kimadini kujitosheleza kwa miundombinu katika mnyororo wa shughuli za madini

" Ninaupongeza sana uongozi wa kiwanda hiki kwa kuona fursa hii kulingana na ukubwa wa Chunya kimadini', " amesema.

Kukamilika kwa kiwanda hicho kunafanya idadi ya viwanda vya kusafisha dhahabu nchini kufikia vinane.



No comments:

Post a Comment