MKOMI AWAKUMBUSHA WATUMISHI WA UMMA KUHUSU WAJIBU WAO KWA WANANCHI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, October 9, 2025

MKOMI AWAKUMBUSHA WATUMISHI WA UMMA KUHUSU WAJIBU WAO KWA WANANCHI.


Na Carlos Claudio, Dodoma.



Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Selemani Mkomi, amewakumbusha watumishi wa umma nchini kutekeleza wajibu wao ipasavyo kwa kuwahudumia wananchi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Akizungumza leo Oktoba 9,2025 jijini Dodoma, Mkomi amesema ni wajibu wa kila mtumishi wa umma kuhakikisha anatoa huduma bora, zenye weledi na heshima kwa wananchi, ambao ndio wateja wakuu wa Serikali.


Amesema katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Mteja kwa mwaka huu, taasisi za umma zinapaswa kutumia fursa hiyo kujitafakari, kujifunza na kuboresha utendaji wao kupitia mrejesho unaotolewa na wananchi.


“Wiki hii iwe ni wakati wa kujipima na kuona wapi tunafanya vizuri na wapi tunapaswa kuboresha. Tuwaangalie wananchi kama wateja wetu muhimu na tusikilize mrejesho wao kwa dhati,” amesema Mkomi.


Ameeleza kuwa taasisi mbalimbali za umma zimekuwa zikishiriki maadhimisho hayo kwa kutoa huduma na kueleza majukumu yao kwa wananchi, jambo linalosaidia kuongeza uwazi na uelewa kwa umma kuhusu huduma zinazotolewa na Serikali.


Kwa mwaka huu, maadhimisho hayo yamebebwa na kaulimbiu isemayo “Dhamira Inayowezekana”, ambayo kwa mujibu wa Mkomi, inamaanisha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa vitendo.


“Serikali yetu ina rasilimali, mipango na sera sahihi zinazolenga kumuinua mwananchi. Ni jukumu la kila mtumishi wa umma kuhakikisha dhamira hii inatekelezwa kwa vitendo,” alisisitiza.



Mkomi amewataka watumishi wa umma kutumia wiki ya huduma kwa mteja kuzingatia wajibu na mamlaka waliyopewa kwa mujibu wa Katiba, akitaja Ibara ya 6 ya Katiba ya mwaka 1977 inayosema kuwa Serikali ni mtu au chombo kinachotekeleza mamlaka kwa niaba ya Serikali.


“Ustawi wa wananchi unapatikana pale ambapo watumishi wa umma wanatekeleza wajibu wao kwa uadilifu, uaminifu na uwajibikaji,” alisema.


Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo ameeleza kuwa watumishi wa umma wenye changamoto za vituo vya kupigia kura kutokana na kuhamishwa kikazi watapewa nafasi ya kushiriki zoezi hilo kwa mujibu wa utaratibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).


“Kwa watumishi ambao hawawezi kupiga kura katika vituo walivyojiandikisha, tume inaruhusu wapige kura ya Rais, japokuwa kura za Mbunge na Diwani hazitahusishwa. Hivyo kila mmoja atumie fursa hii ipasavyo,” amesema Mkomi.


Amefafanua kuwa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja Duniani huanza rasmi tarehe 6 Oktoba na hufikia kilele chake tarehe 10 Oktoba kila mwaka, ambapo taasisi mbalimbali huonesha jitihada zao katika kuboresha huduma kwa wananchi.


Mkomi amehitimisha kwa kuwasihi watumishi wa umma kuendelea kuwa mfano wa uwajibikaji na uadilifu, akisisitiza kuwa ustawi wa wananchi ndio kipimo halisi cha mafanikio ya utumishi wa umma.









No comments:

Post a Comment