TANZANIA KUZINDUA MAABARA ZA KISASA ZA KUPIMA MATUMIZI BORA YA NISHATI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, October 15, 2025

TANZANIA KUZINDUA MAABARA ZA KISASA ZA KUPIMA MATUMIZI BORA YA NISHATI



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaaam


Serikali kwa Kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), kupitia ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) watazindua Viwango Fanisi vya Chini vya Nishati (Minimum Energy Performance Standards – MEPS) na Maabara za Upimaji wa Ufanisi wa Nishati.

Uzinduzi huo utafanyika Oktoba 16,2025, jijini Dar es Salaam katika Makao Makuu ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Kamishna na Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga amesema hayo leo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam ambapo amesema kuwa lengo la kuanzishwa kwa maabara hiyo ni kuhakikisha kuwa vifaa vinavyotumika nchini vinatumia nishati kwa ufanisi kwa lengo la kupunguza gharama kwa watumiaji na kulinda mazingira dhidi ya uzalishaji wa hewa ukaa.

Ameongeza kuwa juhudi hizo zitasaidia kupatikana kwa umeme wa ziada kwenye gridi ya taifa na kutumika katika maeneo mengine ya nchi yenye upungufu wa umeme na kuweza kuwafikia wateja wengine wapya.

Amesema kupitia mradi huo, Tanzania itazindua viwango vya kwanza vya chini vya matumizi ya nishati ya umeme vinavojulikana kama MEPS kwa vifaa vitano vya kipaumbele ambavyo vinachangia matumizi makubwa ya umeme ambavyo ni Viyoyozi Majokofu, Runinga, Feni pamoja na Mota za umeme.

“Watu wengi wamekuwa wakitumia vifaa mbalimbali majumbani na maeneo mengine bila kufahamu kiwango halisi cha umeme kinachotumika katika vifaa, hivyo kuwepo kwa maabara hiyo nchini, kutasaidia kupima vifaa hivyo na kujua matumizi fanisi ya nishati na hivyo kuokoa gharama katika matumizi” Amesema Mha. Luoga

Mha. Luoga amesema kuwa maabara hizo zitakuwa na jukumu la kupima na kuthibitisha ubora na ufanisi wa vifaa vya umeme vinavyoingizwa nchini, kudhibiti bidhaa duni zisizo na viwango,kutoa ithibati kwa wazalishaji wa ndani na kusaidia Serikali katika usimamizi wa soko.

Mha. Luoga amefafanua kuwa maabara hizo zinathamani ya zaidi ya Euro milioni 1.8 (takriban shilingi bilioni 5).

Amesema kwa mara ya kwanza, Tanzania itakuwa na uwezo wa ndani wa kuhakikisha bidhaa zote zinakidhi viwango vya kitaifa na vya kikanda kabla ya kufika kwa mlaji.

Amesema uundaji wa viwango hivyo umehusisha Wataalam kutoka taasisi zaidi ya 10 zikiwemo Wizara ya Nishati, TBS, TANESCO, EWURA, REA, TIRDO, DIT, UDSM, ATC, NCC, TAREA na sekta binafsi.

Ameongeza kuwa kwa ushirikiano wa kitaalamu na Mshauri wa Kimataifa, viwango vya kiyoyozi na majokofu vimeidhinishwa rasmi kuwa viwango vya Kikanda vya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hatua inayowezesha Tanzania kuwa sehemu ya soko la kikanda lenye bidhaa zenye ubora na ufanisi wa nishati.

Uanzishaji wa MEPS na maabara hizi unalenga kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Nishati ya Taifa (2015), Mkakati wa Taifa wa Matumizi Bora ya Nishati (NEES 2024–2034) na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Katika hatua nyingine , Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeanza juhudi za kuandaa viwango katika teknolojia ya kupikia kwa kutumia nishati Safi ili kuendana na Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034).

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upimaji na Huduma za Metrolojia wa TBS, Ridhiwani Matange ametoa wito kwa watanzania kutumia vifaa ambavyo vitakuwa vimepimwa katika maabara hizo.

Amesema elimu zaidi itatolewa kwa wananchi ili kuwajengea uwezo wa uelewa juu ya maabara hizo na viwango fanisi vinavyohitajika katika matumizi yao ya kila siku.

Naye Mkuu wa Ushirikiano wa Umoja wa Ulaya, Arc Stalmans na Msaidizi wa Mwakilishi Mkazi, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Gertrude Lyatuu waamesisitiza kuwa wataendela kushirikina na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hususan mradi huo wa matumizi bora ya nishati ili kupunguza hewa ya ukaa ili kulinda Mazingira.


No comments:

Post a Comment