TARURA YATEKELEZA MIRADI MIKUBWA YA MIUNDOMBINU YA BARABARA YA BILIONI 302.95 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, October 13, 2025

TARURA YATEKELEZA MIRADI MIKUBWA YA MIUNDOMBINU YA BARABARA YA BILIONI 302.95




Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff amesema katika kipindi cha miaka minne (4) ya Serikali ya Awamu ya Sita, Wakala umekamilisha ujenzi wa miradi mikubwa ya miundombinu ya barabara za Wilaya yenye thamani ya Shilingi Bilioni 262.46 huku miradi yenye thamani ya Shillingi Bilioni 40.49 ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji na miradi yote ikikamilika itakuwa na thamani ya Shilingi Bilioni 302.95.

Mhandisi Seff amesema mafanikio hayo yametokana na ongezeko la bajeti lililofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa TARURA ambapo awali walikuwa wakipokea bajeti ya Shilingi Bilioni 275 kwa mwaka lakini baada ya Serikali ya Awamu ya Sita kuona kazi kubwa ya TARURA bajeti iliongezeka kutoka Bilioni 275 kwa mwaka hadi kufikia Shilingi Trilioni 1.1 sawa na ongezeko la asilimia 230.

“Baadhi ya miradi iliyokamilika ni ujenzi wa barabara za lami Kilomita 58.5 katika mji wa Serikali Mtumba-Dodoma, daraja la Berega mita 140 wilayani Kilosa-Morogoro, daraja la Mbwemkuru mita 75 wilayani Ruangwa-Lindi, barabara ya lami Visiga-Zegereni Kilomita 12.5 wilayani Kibaha-Pwani na barabara ya lami Kilomita 5.1 katika eneo la viwanda Dodoma”, amesema.

Ameeleza kuwa, Wakala umeendelea na usimamizi madhubuti wa miradi ya wadau wa maendeleo ya Benki ya Dunia na Umoja wa Nchi za Ulaya. Miradi hiyo ni Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP 2) wenye thamani ya Shilingi Bilioni 1,136.172 {US$ 438 milioni}), Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi (MBD) wenye thamani ya Shilingi Bilioni 608.4 {US$ 260 milioni) na Uboreshaji wa Miji 45 (TACTIC) wenye thamani ya Shilingi Bilioni 959.4 {US$ 410 milioni}).

Miradi mingine ni uboreshaji wa barabara za vijijini na fursa za kijamii na kiuchumi kwenye maeneo yenye fursa za kilimo (RISE) wenye thamani ya Shilingi Bilioni 811.65 {US$ 350 milioni}) na Ujenzi wa barabara kwenye maeneo ya kilimo cha mazao ya Kahawa, Chai, matunda na mbogambaga (Agri-connect) wenye thamani ya Shilingi Bilioni 138.528 {EUR 48 milioni}).

“Miradi hii ikikamilika itagharimu takribani Shilingi Trilioni 3.68 na hadi sasa utekelezaji wa jumla umefikia asilimia 40 na miradi yote inategemewa kukamilika ifikapo mwezi Aprili 2030. Miradi hii ikikamilika jumla ya Kilomita 1,242.52 za barabara za lami, Kilomita 151 za mifereji, masoko 56 na stendi za mabasi 39 vitakuwa vimejengwa”, ameongeza.

Aidha, Mhandisi Seff amesema Wakala umetekeleza miradi ya ujenzi na matengenezo ya barabara za Wilaya kwa kuzingatia sera za ushiriki, ushirikishwaji na uwezeshaji wa jamii kiuchumi ambapo asilimia 99.2 ya zabuni za ujenzi na matengenezo ya barabara za vijijini na mijini zimekuwa zikitolewa kwa makandarasi wazawa kila mwaka huku asilimia 30 ya bajeti ya Mfuko wa Barabara hutumika kutoa zabuni kwa makundi maalumu kila mwaka.

“Jumla ya vikundi 344 vya wananchi vimeshiriki kwenye kazi za matengenezo ya barabara na hadi kufikia Julai, 2025 ajira 173,760 zilitolewa kwa wananchi kwenye miradi ya ujenzi wa barabara”, amesema.

Vilevile, ameongeza kuwa Wakala kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (Economic and Social Research Foundation-ESRF), umefanya tathmini ya matokeo ya uboreshaji wa barabara za vijijini na ufikiwaji wake kwa wananchi, mwaka 2025. Tathmini hiyo imeonesha matokeo makubwa yaliyopatikana baada uboreshaji wa mtandao wa barabara za Wilaya.

“Tathmini imeonesha, muda wa usafiri na usafirishaji kwenda kwenye huduma za kijamii na kiuchumi kama masoko na hospitali umepungua kwa dakika 17.5, gharama za usafiri na usafirishaji zimepungua kwa asilimia 75.3, hali ya upatikanaji wa usafiri na usafirishaji imefikia asilimia 86 ikilinganishwa na asilimia 20 kwa barabara ambazo hazijaboreshwa na endapo barabara zikiboreshwa kwa kiwango cha lami au changarawe hali ya usafiri inaongezeka kwa takribani asilimia 66 na upotevu wa mazao umepungua kwa asilimia 72.5 kutokana na uboreshaji wa barabara vijijini”.

Ameendelea kufafanua “kiwango cha ufikiwaji wa mtandao wa barabara za Vijijini unaopitika majira yote ya mwaka kimeongezeka kutoka asilimia 24.6 mwaka 2016 hadi asilimia 61.0 mwaka 2025, hii inaonesha kwamba sehemu kubwa ya wakazi wa vijijini wana pata huduma za usafiri na usafirishaji jambo ambalo ni muhimu kupunguza umasikini, upatikanaji wa huduma na ukuaji wa Uchumi”.

Katika hatua zilizochukuliwa kukabiliana na changamoto za mitaji kwa Makandarasi Wazawa katika kutekeleza kazi za barabara za Wilaya, Mhandisi Seff ameeleza kuwa Wakala kwa kushirikiana na Benki ya CRDB imeratibu uanzishwaji wa Hati Fungani ya Miundombinu iitwayo “SAMIA INFRASTRUCTURE BOND” kwa lengo la kukusanya jumla ya Shilingi Bilioni 150 ili kuwasaidia Wakandarasi wazawa kupata fursa za mikopo ya fedha na dhamana za kazi kwa gharama nafuu.

“Kiasi cha Shilingi Bilioni 323.09 zimekusanywa ikiwa ni asilimia 215.4 ya lengo lililowekwa ambapo kiasi cha Shilingi Bilioni 223.8 kimeombwa na Wakandarasi Wazawa wapatao 276 kwa ajili ya utekelezaji wa kazi za mikataba ya matengenezo na ujenzi wa barabara”.

No comments:

Post a Comment