
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kujenga Uwanja wa ndege Mugumu Serengeti kama sehemu ya kutimiza adhma ya Chama Cha Mapinduzi ya kufikisha idadi ya watalii Milioni nane wanaoitembelea Tanzania kwa mwaka kufikia mwaka 2030.
Dkt. Samia ameahidi pia kuendelea kutangaza vivutio na kukuza utalii wa Tanzania, akiitaja hifadhi ya Taifa Serengeti kama nguzo muhimu ya Utalii nchini kutokana na namna inavyoendelea kuitangaza Tanzania Kimataifa ikichukua tuzo mara tatu mtawalia kama Hifadhi bora duniani.
"Mji huu wa Serengeti una umuhimu na fursa kubwa za uwekezaji wa hoteli za utalii kwakuwa upo katikati ya maeneo yaliyohifadhiwa kwa wageni wanaotoka Sirari na Seronera kwenda Kogatende, Kaskazini mwa hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambapo pia kuna utalii wa nyumbu wanaohama kwenye Ikolojia ya Serengeti." Amesema Dkt. Samia.
Dkt. Samia amehitimisha Mikutano yake ya Kampeni Mkoani Mara na kurejea tena Mkoani Simiyu kuendelea na Kampeni zake kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akisisitiza pia kuongeza kasi katika kuhudumia jamii dhidi ya mahitaji yao ya msingi ikiwemo afya, elimu, maji, kilimo, miundombinu ya barabara na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.



No comments:
Post a Comment