
Akiwa Mkoani Kilimanjaro leo Jumatano Oktoba Mosi, 2025 kwenye muendelezo wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu, Mgombea wa nafasi ya Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuwa ikiwa atapewa ridhaa ya kuunda serikali, atafufua na kuendeleza Viwanda vyote vya Kanda ya Kaskazini ikiwemo vya Mkoa wa Kilimanjaro, viwanda ambavyo vilibinafsishwa na baadaye kushindwa kuendelea na uzalishaji.
Dkt. Samia ameyaeleza hayo Moshi Mjini kwenye Viwanja vya Mashujaa, akiwa kwenye siku yake ya Pili ya Kampeni Mkoani Kilimanjaro kabla ya kuelekea Mkoani Arusha, akisema kufa kwa viwanda hivyo kumesababisha ukosefu wa ajira kwa Vijana pamoja na kufifia kwa shughuli za uchumi na uzalishaji kwenye Mikoa mingi nchini.
Mgombea huyo wa Urais na wa kwanza mwanamke kuwania nafasi hiyo ndani ya Chama Cha Mapinduzi, ameahidi pia kuendelea kukiwezesha Kiwanda cha Kilimanjaro Machine Tools cha Wilayani Hai ili kiweze kuzalisha zaidi bidhaa zake zinazohudumia Viwanda vingine nchini, akisema kuanza uvunaji wa Chuma na Makaa ya mawe kwenye mradi wa Liganga na Mchuchuma kutawezesha upatikanaji wa malighafi za kutosha katika kuhudumia Kiwanda hicho pamoja na Viwanda vingine nchini.
Kuhusu Mradi wa Liganga na Mchuchuma Dkt. Samia amewaambia wananchi wa Kilimanjaro kuwa mradi huo upo katika hatua za mwisho ili kuanza uchimbaji wake, akieleza kuwa kwasasa serikali inamalizia mazungumzo na muwekezaji ili kuweza kuanza kazi kwa mradi huo muhimu na wa kimkakati nchini Tanzania






No comments:
Post a Comment